MKUU wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa mradi wa ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ya wilaya hiyo lililogharimu Sh. milioni 278 ambalo ujenzi wake umeonekana kuwa chini ya viwango kabla ya kuanza kutumika.
Akizungumza na watumishi na viongozi wa hospital hiyo mara baada kutembelea na kukagua jengo hilo kwa mara ya pili mwishoni mwa wiki, Shaka amesema mradi huo una madudu mengi na kuagiza kufanyika kwa uchunguzi.
Amesema jengo limejengwa chini ya viwango na tangu aagize kufanyike marekebisho mpaka sasa wameshindwa kukamilisha kwa wakati bila sababu za msingi.
“Fedha zimeletwa zaidi ya Sh. milioni 200 katika mradi huu lakini cha kusikitisha viongozi mmeshimdwa kujitambua, umakini na kusimamia jukumu hili, pamoja na yote mnaniambia hata mjenzi wa awali mliyempa kazi na kuharibu hamumjui mtampata wapi, mambo ya ajabu sana, haiwezekani kabisa ndio maana ninataka vyombo vyote vya ulinzi na usalama vilivyopo hapa kila chombo kibebe jukumu lake nataka nipatiwe taarifa ya uchunguzi na watafutwe kila aliyehusika kwenye uzembe huu ifikapo Jumatano,”amesema Shaka na kuongeza kuwa:
“Nielezwe ni nini kinachoendelea TAKUKURU mpo hapa, jeshi la polisi mpo hapa na vyombo vingine kila mmoja afanye jukumu lake itakavyofika Jumatano ninataka taarifa tumechoka hizi hadithi ukienda ukirudi unapatiwa hadithi nyingine embu angalia kile nini? msicheze na fedha ya Serikali nia ya moto,”
Shaka alishangazwa na jinsi ambavyo vifaa vilivyotumika katika jengo hilo kuwa vya kuunga unga na vyengine vikikosa ubora, uimara pamoja kuweka saruji katika paa za jengo hilo jambo ambalo limesabisha jengo hilo kuvujisha na maji kuingia ndani kuharibu taswira ya jengo.
“Ina maana huyu ameenda dukani kuomba vipande vipande mikanda ya gpsum ndio amekuja kutuwekea hapa, huwezi kusema hii mikanda imekuja kwenye jengo la serikali alafu kafanya hivi kwa jengo nzima viongozi mpo mnangalia mnaona ni sawa tu kuna shida hapa,” amesema Shaka
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED