WASIWASI ni jambo ambalo kila mwanadamu ameumbwa nalo. Hakuna mtu asiyekuwa na wasiwasi kwa sababu lazima awaye yote lazima awe na shaka juu ya kitu fulani kama wahenga wasemavyo si yote yang’aayo ni dhahabu.
Kutokana na ukweli huo, mtu kabla hajaliendea jambo kulifanya, ni lazima awe na shaka au wasiwasi. Aidha, kuna msemo au methali kwamba barabara ndefu haikosi kona, hivyo hata kama kuna uhakika na jambo fulani, lazima wasiwasi uwapo.
Pamoja na ukweli huo, wataalam wa saikolojia wamesema hofu au wasiwasi uliopitiliza ni tatizo la afya ya akili na lisiposhughulikiwa mapema linaweza kusababisha athari za kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, licha ya hali ya wasiwasi kuwa ni muhimu kwa ustawi wa mwanadamu kwa kuongeza ari ya kujishughulisha, ikizidi inaweza kusababisha kuleta madhara hasi ikiwamo kujiua.
Kutokana na hali hiyo, wameshauri kuwa mtu akihisi kuwa na dalili za wasiwasi uliopitiliza, aonane na mtaalamu wa saikolojia ili kukabiliana na tatizo hilo kabla halijawa kubwa ma kuleta athari.
Mwanasaikolojiatiba Dk. Saldin Kimangale, anasema hofu au wasiwasi inachukuliwa kama ni ugonjwa wa afya ya akili kama itadumu kwa muda mrefu kiasi cha kuingilia utendaji wa kazi wa mtu ikiwamo kifamilia, kibiashara na uhusiano. Pia anasema hali hiyo inaweza kuwa changamoto ya afya ya akili.
Anasema watu wenye magonjwa ya wasiwasi huwa wameelemewa na hali ya kuwa na hofu isiyo na sababu au chanzo maalumu.
"Magonjwa ya wasiwasi yameenea sana. Kwa kila watu wazima watano, walau mtu mmoja atapata ugonjwa huo kila mwaka. Magonjwa ya wasiwasi yanaweza kukuweka katika hatari ya kupata magonjwa mengine kama vile kisukari na magonjwa mengine yasiyoambukiza, matumizi ya dawa za kulevya na sonona.
“Mtu mwingine ambaye ana tatizo hilo anaweza kujiingiza katika unywaji wa pombe wa kupitiliza na hata kuhatarisha afya yake hasa anapotumia vilevi vikali. Bahati nzuri matibabu ya magonjwa ya wasiwasi yapo," anasema
“Tunapokabiliwa na vitisho, kwa kawaida ubongo hupokea taarifa, ikaichakata kisha ikapeleka amri kwa mwili nini cha kufanya ama kupambana, kukimbia au kushikwa na butwaa,” anasema.
NINI CHANZO?
Mtaalamu huyo anasema ili wasiwasi au hofu itokee, homoni zijulikanazo kama ‘adrenalin’ na ‘kotisol’ humwagwa kwa ajili ya kupeleka nguvu kwenye misuli tayari kuikabili hatari na iwapo hatari ipo kweli, basi kunapatikana uwiano baina ya kitisho na hatua ya kuchukua.
Anasema tatizo linakuja pale ubongo unapobeba taarifa za kitisho, kitu ambacho hakipo au si cha kweli, kisha ikauandaa mwili kwa mapambano lakini hakuna kitisho halisi ndipo hapo mwili unapojigeukia wenyewe.
"Unaweza kukisia ni kwa kiwango gani mwenye ugonjwa wa wasiwasi anavyoteseka kwa namna ambavyo wakati wote akili inatuma ujumbe wa kutambua hatari kimakosa na kuuandaa mwili kukabiliana na kitisho hicho kisichokuwapo. Mtu anadumu katika hali hiyo usiku na mchana kwa siku nyingi, wiki na hata miezi au mwaka," anasema.
ATHARI KIUCHUMI
Mtaalam wa saikolojia na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tuwainue Foundation, Dk. Dismas Lyassa, anasema mtu mwenye hali ya uoga au tabia ya kuwa na wasiwasi, anaweza kupata athari mbalimbali ikiwamo kupungua ufanisi wake katika kazi.
Anasema wasiwasi na hofu mara nyingi husababisha mtu kushindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi hali ambayo inaweza kusababisha kupungukiwa na tija kazini, hivyo kupunguza uwezo wa kuongeza mapato au kupata vyeo vya juu.
"Wasiwasi na hofu vinaweza kumfanya mtu kuwa na shaka kuhusu uamuzi wake wa kifedha kama vile uwekezaji, matumizi ya fedha au kuanzisha biashara. Hii inaweza kusababisha uamuzi mbaya wa kifedha kama vile kupoteza fedha au kukosa fursa muhimu za kibiashara," anasema Dk. Lyassa.
Anataja madhara mengine ni ya afya. Mtu mwenye tatizo au ugonjwa wa wasiwasi, anaweza kupata athari za kiafya na matokeo yake atatumia muda mwingi na gharama nyingi kwa ajili ya matibabu.
“Hali ya uoga au hofu inaweza kusababisha matatizo ya kiafya kama vile shinikizo la damu, matatizo ya usingizi, au matatizo ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula, hivyo kutumia pesa nyingi kujitibia.
Anaongeza kuwa mtu mwenye wasiwasi au hofu anaweza kuwa na uoga wa kuchukua hatua au kujiunga na fursa mpya za ajira au biashara hali inayoweza kumfanya apuuzie mbali fursa za kuboresha hali yake ya kifedha, hivyo kujikuta nyuma kimaisha.
Pia anasema wasiwasi unaweza kumfanya mtu kuwa na ugumu wa kupanga na kufuata mipango ya kifedha na kumzuia kufikia malengo yake ya kifedha kama vile kuokoa fedha, kumiliki nyumba au kuanzisha biashara.
Kwa mujibu wa Dk. Lyassa, ugonjwa huo unaweza pia kuathiri uhusiano wa kifamilia na kijamii kwa kuwa mtu mwenye hali hiyo mara nyingi huwa na shida za kushirikiana na wengine au kuzungumza kuhusu hali yake. Hatua hiyo, anasema husababisha migogoro ya kifedha ndani ya familia au hata kupunguza msaada wa kifedha kutoka kwa familia na marafiki.
Anashauri watu wanaohisi kuwa wana dalili za ugonjwa huo kutafuta msaada wa kisaikolojia au kufuata mbinu za kupunguza wasiwasi ili kuboresha hali yake ya kiuchumi.
ASHUHUDIA
Maria Lameck, mkazi wa Mbezi Malamba Mawili, mkoani Dar es Salaam, anasema alipitia hali ya kuwa na wasiwasi uliopitiliza kwa muda mrefu bila ya kujua kuwa ana shida ya afya akili.
Kwa mujibu wa Lameck, hali hiyo ilisababisha wakati fulani akashindwa hata kujumuika na wenzake katika masuala mbalimbali ya kijamii.
Kwa mujibu wa Lameck, hali hiyo ilimtokea baada ya kufanyiwa operesheni na kuondolewa titi lake la upande wa kushoto baada ya kukutwa na vimelea vya ugonjwa wa saratani.
"Baada ya kukatwa nikawa na hofu kupitiliza. Kikubwa nilikuwa sitaki kuchangamana na watu nikihofu kuwa labda wataniona kama siyo mwenzao.
“Hatua hiyo ilinifanya niliishi na hali hii kwa mwaka mzima mpaka pale nilipoamua mwenyewe kumwona daktari na kumweleza naye akanipeleka kwa daktari wa afya ya akili," anasimulia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED