UNAPOTEMBEA katika Mitaa ya Agrey, Nyamwezi, Livingstone, Swahili na Congo jijini Dar es Salaam, ni kawaida kuona raia wa kigeni wakifanya kazi ambazo zinapaswa kufanywa na Watanzania na wao kufanya kazi za kitaalamu na uwekezaji.
Hawa wageni wanapaswa kuwapo katika kazi za kitaalam na uwekezaji mkubwa, huku wakitakiwa kutekeleza majukumu yao katika kazi za kitaaluma.
Raia hao wenye asili ya China hutumia mbinu mbalimbali zikiwamo kuwa na maduka ambayo huonyesha wanauza bidhaa kwa jumla, lakini hugeuka kuwa wauzaji wa rejareja na wakati mwingine huchuuza bidhaa kutoka eneo moja hadi jingine la jiji la Dar Es Salaam.
Hivi karibuni, palizuka mgogoro baina ya raia wa China na Mtanzania wakigombea eneo la kupanga bidhaa zao.
Picha jongefu za tukio hilo zilisambaa kwa kasi kubwa kwenye mitaandao ya kijamii hatua iliyomshtua Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye aliagiza mamlaka za serikali kuhakikisha raia wa kigeni wanafanyakazi kwa mujibu wa vibali vyao, huku akitaka kazi za Watanzania kulindwa.
Aidha, alitoa maelekezo kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Seleman Jafo, “Nimeona video Mchina akipigana na mwenyeji tena mwanamke, mchina mwanaume na mwenyeji mwanamke, ngumu za kweli kweli, nilipouliza kulikoni nikaambiwa yule Mchina naye anauza mitumba, biashara ya wenyeji, tena wenyeji vijana wetu. Hilo nalo kalitizame”.
“Kama biashara haifai kufanywa na watu wa nje wasifanye, sababu ni nini mpaka wanapewa leseni ya kufanyabiashara za aina ile, na kama hawapewi leseni kwanini wanafanyabiashara za aina ile.”
Mfanyabiashara katika soko hilo, Yusufu Charles anasema mwingiliano huo unawagharimu kibiashara kwa kuwa Wachina wanauza kwa bei ya rejareja tena kwa bei ndogo kuliko wazawa kwa kuwa wana mitaji mikubwa na bidhaa wanazitoa nchini mwao kwa bei ya chini.
Anasema Wachina wanatakiwa waje kama wawekezaji wakubwa, wauze bidhaa zao kwa bei ya jumla, lakini sio kuchanganyika sokoni kama machinga.
Aidha, anasema kujipenyeza kwao katika soko hilo kumetokana na viongozi wenye mamlaka kutowajibika ipasavyo na kuendekeza rushwa.
“Wapo mpaka waliogeuka kama machinga, walianza kidogo kidogo, sasa wameongezeka wengine wanajifanya wana maduka ya jumla, lakini ukienda dukani wanauza kwa bei ya rejareja.
“Ninaona mwingiliano huu kwa sasa kuudhibiti itakuwa ngumu kwa sababu wanajua njia zote za kuikwepa serikali na wanafundishwa na wazawa waliowaajiri katika maduka yao.
“Kingine wanachokifanya kwa kuwa wanajua sheria haiwaruhusu wao kufanya biashara kama wafanyabiashara wadogo, wanatumia kivuli cha wazawa kumiliki maduka ili isiwe rahisi wao kutambulika,” anafichua Charles
Anaendelea, kutanabaisha kwamba “ukiingia katika duka la mchina hata ukitaka kijiko au kikombe kimoja unapata wakati wao wanatakiwa kuuza kuanzia dazani moja na kuendelea”.
Mfanyabiashara mwingine Rashid Chunga, anashauri Wachina wote waondolewe katika soko hilo na baadala yake wapatiwe sehemu pembezoni ya jiji wakawekeze huko.
“Biashara ambazo ni mahsusi kufanywa na wazawa zinafanywa na Wachina, hali inazidi kuwa mbaya kwa Watanzania ndio maana kila siku malalamiko ya kukosa ajira yanakuwa mengi.
“Wanatuua kibiashara, wanavuruga ushiriki wa wazawa katika kujenga uchumi wa nchi yao na sasa tunashuhudia baadhi ya wazawa wanafunga maduka kwa sababu kushindana na mchina kibiashara sio rahisi wana mbinu nyingi na wana mitaji mikubwa.”
“Ukituuliza leo tunataka nini kuhusu Wachina, nitakwambia tunataka wawe Kimanzichana, Kibaha, Chamanzi, Mkuranga mfanyabiashara atoke hapa awafuate huko akafunge bidhaa arudi sio kuwa nao hapa, tena wakiuza kwa rejareja”.
Kwa Wachina kwenda pembezoni mwa jiji, “sio tu itapanua wigo wa kibiashara pia itapunguza msongamano uliopo Kariakoo, wakati mwingine hata kutupunguzia bei katika bidhaa zao wanashindwa kwa sababu tupo nao hapahapa wanajua bei halisi yaani kama wazaramo wenzetu tu,” analalamika.
Mariam Ngonyani mfanyabiashara wa mitumba anasema anaona kuna hasara katika hilo akiwa na ufafanuzi kwamba:
“Wachina hawanunui bidhaa nchini, kazi yao ni kukusanya fedha za zetu na kuzibadilisha kuwa dola halafu wanazipeleka nchini kwao, kwa hiyo ukiangalia kwa picha kubwa unagundua hawasaidii kujenga uchumi wa Tanzania badala yake wanauvuruga kwa faida yao”.
“Waende nje ya mji wasiruhusiwe hata kuwa na maduka ya jumla wengi pia wanapitia mwanya huo, baadaye wanaanza kuuza kwa bei ya rejareja sasa hivi tunaishi nao wanajua mpaka namna ya kukwepa kodi wakati mwingine hata risiti hawatoi wamebadilika.
Irene Nzala mfafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi anafichua njia nyingine wanayiotumia kumiliki maduka na kuuza kwa rejareja kwamba huwa wanatafuta wazawa ambao wana mitaji midogo halafu wanakubalina kufanya biashara pamoja.
“Unakuta mara ghafla mtu duka lake limejaa, ukipeleleza vizuri unakuta asilimia 80 ya bidhaa zilizopo ni za mchina, wao hawataki kujulikana bali mchina huyo anaonekana muda wa kufunga hesabu tu,” anasema Irene huku akizitaka mamlaka za serikali zinazohusika na viwanda na biashara na Mambo ya Ndani kuziba mianya ya leseni na vibali kwa wageni.
Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Uroki Ombeni, anathibitisha kuwapo kwa changamoto hiyo akiwa na ufafanuzi kwamba kitendo cha Wachina kuingilia biashara za wazawa ni kufanya Watanzania waendelee kubaki masikini na ombaomba.
Anasema kila siku wananchi wanaendelea kutumbukia katika dimbwi la umasikini serikali inaona lakini hajui kwanini hakuna hatua inayochukuliwa hii inaweza kuleta athari kubwa sana baadaye.
Ombeni anashauri serikali iangalie namna ya kupunguza kasi ya wachina kuingia katika soko hilo, akisisitiza iwapo hali itaendelea kuwa hivyo italeta hatari kwa maendeleo ya nchi na uchumi kwa wafanyabiashara.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana anaungana na mtangulizi wake Ombeni akiwa na la ziada kwamba changamoto hiyo ni kubwa ukizingatia asilimia 85 ya bidhaa zinaagizwa China.
Anasema ni ngumu kushindana nao kibiashara akiwa na ufafanuzi kwamba “Wao (Wachina) wanapata faida mara mbili, kwa kuwa tunanunua katika maduka yao na viwanda vyao, lakini wao tena wanakuja huku wanapenya huku kwa ujanja ujanja wanafungua maduka wanauza kwa rejareja.
“Kwa akili ya kawaida hatuwezi kushindana nao kwa sababu kwanza wao bidhaa nyingi zinatoka kwao, wanapata kwa bei ndogo, wanakopeshwa na viwanda vya kwao kwa bei ya chini na riba ndogo ndio maana wanauza kwa bei ya chini na wanapata faida,” anasema Mbwana.
“Kipindi cha nyuma tuliona kulikuwa na mkazo wa kufuatilia kibali, lakini kwa sasa si ajabu kuona mchina yuko dukani anauza na watu wa uhamiaji wanapita wanaona na hawafanyi kitu chochote jambo hili linaleta picha mbaya kwa wanan hi hasa wafanyabiashara dhidi ya serikali yao,” anahadharisha Mwenyekiti Mbwana.
Anaendela na ufafanuzi wake kwamba upo ujanja mwingine wanaotumia wachina wa kuingia ubia na wazawa na kuwaweka mbele ya biashara zao.
Anasema baadhi ya maduka yanauza bidhaa kwa bei ya rejareja lakini yanamilikiwa na Wachina, kwamba wanajificha katika kivuli cha wazawa, lakini katika usajili na mambo ya kibenki hausishi. Mtanzania serikali iliangalie na hili pia.
“Lengo la kubwa la Wachina ni kushika soko la Afrika Mashariki, tusipopigia kelele suala hili mapema itafanya baadaye Watanzaia wawe watumwa wao wakati sisi ndio wenye nchi,” anasema.
Aidha, Mwenyekiti huyo, anashauri suala hilo lidhibitiwe mapema baadaye wakiwa wengi itakuwa ngumu kuwaondoa yataanza mambo ya kidiplomasia itaonekana tunavunja haki za biandamu, lakini sisi lazima tuthamini vya kwetu, kwa sababu hata wao wako makini kulinda vya kwao na wanauzalendo mkubwa.
Uchunguzi wa gazeti uliofanywa katika nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki unaonesha kuwa huko kwingine kuna udhibiti mkubwa dhidi ya wageni kufanya biashara ambazo zinaweza kufanywa na wazawa.
Mamlaka za Tanzania zinapawa kulinda wananchi wake dhidi ya wageni wanaokuja kuchukua kazi ambazo zinaweza kufanywa na wazawa, kwa kuwa likiachwe likaendelea itakuwa inatengeza bomu ambalo haitakuwa rahisi kulithibiti.
“Sisi tunapenda wachina waje na ujuzi tuige teknolojia yao, waje kama wawekezaji, lakini sio kama ilivyo kwa sasa Kariakoo hii si ishara nzuri kwa kizazi cha baadaye” anafafanua.
Mbwana anashauri Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kufanya ziara na kwamba wako tayari kuwapa ushirikiano iundwe timu ya pomoja kwa ajili ya kufuatilia suala hilo.
Alipuulizwa migogoro mingapi ilifika ofisini kwake inayotokana na mwingiliano wa kibiashara kati ya Wachina na wazawa, anasema ameshawahi kusuhuhisha mitatu na kwamba anaona kuna hatari kubwa mbele yake kama suala hili halitapatiwa ufumbuzi.
Ofisa Biashara Jiji la Dar es Salaam, Nikasi Msemwa anasema changamoto tajwa haiko kwa Wachina pekee, bali wapo hata watu kutoka mataifa mengine wanaofanya hivyo.
“Leseni tunazowapatia zinaelekeza wawe wafanyabiashara wa jumla sio rejareja, tuliwahi kupata hayo malalamiko tukawaandikia barua, jumuiya ya wafanyabiashara tukawauliza mnawafahamu hao watu? hebu tupeni majina na wao walikuwa hawawafahamu.
“Tumefanya kazi na wahusika na hajaonekana mtu kama huyo, rai yangu kila mfanyabiashara afanye biashara kulingana na leseni aliyonayo,” anasisistiza Msemwa.
Hata hivyo, pamoja na kauli ya Msemwa kwamba hawakufanikiwa kuwapata wanaouza rejareja, uchunguzi wa Nipashe kupitia mwandishi wake aliyepita katika baadhi ya maduka yanayomilikiwa na Wachina na kujifanya kama muhitaji wa huduma alibaini wengi wanauza rejareja.
MADHARA KIUCHUMI
Mchumi na Mtaalamu wa masuala ya fedha wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Prof. Marcellina Chijoriga, anasema mwingiliano huo una atahari za moja kwa moja katika uchumi wa nchi.
“Kisera sio sawa, wageni kufanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania. Jambo hili linaathari za moja kwa moja kiuchumi kwamba wafanyabiashara wa kitanzania watakosa kipato,” anasema Prof. Marcellina.
Hata hivyo, anaonya wafanyabishara wa Kitanzania kuacha kulalamika bali wanapaswa kuwa wabunifu na kujituma na anasisitiza kitu kingine wanachotuzidi wachina ni kuheshimu kazi wanayoifanya.
Anaitaja kasoro nyingine kwa wazawa kwamba wengi wao sio waaminifu kwa hiyo hawawezi kuwa na mitaji mikubbwa kwa sababu hawakopesheki ndio maana lawama zinazidi kila siku.
Mchumi mwingine kutoka Taasisi ya Uongozi na Ujasiriamali (IMED), Dk. Donath Olomi anaungana na mtangulizi akiwa na hoja mbadala kwamba kazi kubwa ya serikali ni kuweka usawa katika biashara.
Anasisitiza jambo hilo, linatakiwa liangaliwe kuna baadhi ya shughuli zinatakiwa zifanywe na Watanzania kama maduka ya rejareja na jumla kwa kuwa hizo hazihitaji mtaji mkubwa au mwekezaji kutoka nje.
“Lakini yapo maeneo kama viwanda tunahitaji wawekezaji kwa sababu Watanzania hatuna utaalamau wa kuviendesha tofauti na wenzetu.
Alipoulizwa kuhusu madhara ambayo nchi inaweza kuyapata kutokana na mwingiliano huo Dk. Olomi alisema: “Inawezekana ukitazama kwa uchumi mkubwa unaweza usione athari kwa sababu unahitaji watu wafanye biashara walipe kodi, lakini matatizo ni kwamba ukitaka kujenga uchumi imara inapaswa sehemu kubwa ishikwe na wazawa.
“Ukiwa na uchumi unaotegemea watu wa nje ni kwamba huo uchumi una shaka sana, kwa sababu hauwafaidishi watu wao, ni kweli kodi inapatikana lakini inahitajika watu wajifunze kufanya biashara wakuze mitaji yao na hiyo ndio namna ya kukuza uchumi imara,” anafafanua Dk. Olomi
Anaendela na ufafanuzi wake kwamba ukitaka kuwa na uchumi imara unahitaji wananchi wake wawe sehemu ya huo uchumi.
“Lakini pia unakuwa na usalama zaidi kwa sababu ikitokea shida kidogo katika biashara kimataifa unaweza kukuta hao wote wakaondoka hata ile huduma uliyokuwa unaipata itapotea.
“Sio kwamba tuwaondoe Wachina wanatakiwa kubaki kama wawekezaji, bila hivyo Watanzania watawekwa pembeni wakati tunataka kujenga taifa ambalo wao watakuwa sehemu ya huo uchumi.
“Hii itasaidia kuepusha wafanyabiashara kufanya maandamano kwa kuanza kupaza sauti …ooh nchi hii imeshikwa na Wachina ili kuepusha vitu kama hivyo tunapaswa kuanza mapema,” alihadharisha Dk. Olomi
Anasema serikali inapaswa kuweka mipango mkakati ya kudhibiti hilo sio kuwafukuza waliopo wakifanya hivyo wataibua mtafaruku mkubwa kwa sababu na sisi pia kuwa Watanzania wanafanya biashara nchini kwao.
“Waliopo wasifukuzawe lakini iangaliwe njia nyingine ya kutenga baadhi ya sera kwa kampuni za kitanzania na wachina.
Tunakokwenda uchumi wa nchi unazidi kukua tukiacha mamabo yaendelee hivi huko tunakokwenda mambo yatakuwa mabaya zaidi,” anasema.
HATUA SERIKALINI
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe anapotolea ufafanuzi hoja hizo anasema wanajitahidi kulinda makubaliano na mwekezaji inapotokea ameenda kinyume huwa wanachukua hatua za kisheria haraka.
“Kwa kweli tusingependa anayekuja kama mwekezaji aje kufanya shughuli za wazawa, tatizo wengi wanageuka kinyemela na kuanza kufanya biashara kinyume na makubaliano huwa tunafuatilia na tunapobaini tunachukua haraka hatua za kisheria.
“Kuhusu hao Wachina tatizo letu tunachanganya huenda wengine walikuja kufanya kazi katika miradi mikubwa baadaye akatafuta namna nyingine kwa kibali maalum halafu akaamua kufanya biashara huyo anakuwa siyo mwekezaji anatambuulika kama anafanya shughuli zake kihalali. (hapa akitaja idadi ya hao wanaojigeuza ingependeza zaidi Salome)
“Ila kama amegeuka bila kufuata utaratibu huwa tunachukua hatua za kisheria haraka na wapo baadhi ambao tumesha wachukulia hatua hizo,” anfafanua Kigahe.(je wako waliofukuzwa nchini kwa kukiuka vibali vyao vya kazi au ukazi nchini baada ya kutumbukia katika biashara)
Hata hivyo, Kigahe anaunga mkono hoja ya wafanya biashara kwamba Wachina watafutiwe sehemu pembezoni akiahidi ushauri huo utafanyiwa kazi mapema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED