RIPOTI MAALUM: Mhitimu shahada ya uzamili aliyegeukia biashara kupika

By Restuta James , Nipashe Jumapili
Published at 07:25 AM Nov 24 2024
Ester Mgidula (26), mhitimu wa Shahada ya Uzamili ya Kiswahili.
Picha:Restuta James
Ester Mgidula (26), mhitimu wa Shahada ya Uzamili ya Kiswahili.

UHABA wa ajira nchini bado ni tatizo. Baadhi ya wanasiasa walishasema ni bomu linaloweza kulipuka wakati wowote. Ni jambo ambalo si tu limeongeza umaskini bali hata baadhi ya watu kuamua kujitoa uhai kwa sababu ya msongo wa mawazo uliosababishwa na ukosefu wa ajira.

Baadhi ya wahitimu wako mitaani wanarandaranda kusaka ajira. Hata baadhi ya walioajiriwa hawafanyi kazi kulingana na fani walizozisomea. 

Ester Mgidula (26), mhitimu wa Shahada ya Uzamili ya Kiswahili mwenye ufaulu wa juu, akiwa na alama (GPA) ya 4.0 kwa shahada na GPA ya 4.6 (uzamili) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ni mmoja wa vijana wa Tanzania wanaotafuta ajira au kujiajiri kupitia fani walizosomea na si kufanya shughuli nje ya taaluma.

Tofauti na malengo yake, Mgidula  yuko mtaani bila ajira, hivyo kulazimika  kujikita kwenye ujasiriamali wa chakula, akipika na kukiuza kupitia mitandao ya kijamii.

Mkazo wa matumizi ya Lugha ya Kiswahili na fursa zinazoambatana nazo ikiwamo kufundisha nje ya mipaka, uliwekwa zaidi kuanzia serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli.

Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa mstari wa mbele kuendeleza na kukuza Kiswahili. Mwaka  jana katika Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, alihutubia kwa Kiswahili.

SAFARI YAKE 

Akisimulia historia yake, anasema alihitimu shahada ya kwanza mwaka 2021 na kupata ufaulu mzuri, lakini kila anapoomba kazi hapati.

“Kwa mfano, chuo kikuu wakitangaza nafasi wanataka watu wawili au mmoja tu na unakuta sisi tumemaliza wengi, hivyo inakuwa ni bahati kupata,” anasema.

Mgidula ambaye ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto watatu, anasimulia kuwa alipomaliza kusoma, kazi ilikuwa kupata ajira, hivyo katika kuhangaika, amewahi kufanya kazi ya kujitolea katika moja ya kampuni za magazeti nchini.

“Wakati ninaendelea na kazi ya kujitolea katika kampuni hiyo mwaka 2021, nikapata ufadhili wa kuendelea kusoma kwa hiyo nikarudi UDSM kwa masomo ya uzamili,” anasema huku akibainisha kuwa amesomea kufundisha Kiswahili kwa wageni, utunzi wa vitabu, uandishi wa miswada, uhariri na uhakiki wa maandiko.

“Nilipomaliza nilitafuta kazi na nikawaza namna nitakavyotumia elimu yangu kufanya kile hasa nilichosomea. Kuna vikwazo vingi na kikubwa ni mtaji. Kwa hiyo nikaona nianze kupika na kuuza chakula, wakati nikitafuta ajira na mtaji wa kufanya mambo makubwa zaidi kwa nilichokisomea” anasema.

Chakula  anachopika, anasema  anakiuza mtandaoni (online) na wateja wake wengi huagiza ndipo hupika. Anasema alianza kazi hiyo Juni, mwaka huu, kwa mtaji wa Sh. 200,000 na hadi sasa umefikia Sh. 400,000.

Anasifu kuwa kufundisha Kiswahili kwa wageni ni kozi nzuri lakini changamoto yake ni upatikanaji wa mtaji wa kuanzisha kituo cha kufundisha somo hilo.

AJIRA NAFASI MBILI

 Mgidula anasema nafasi za kufundisha chuo kwa mwaka zimekuwa zikitoka mbili au moja na wakiomba kufundisha sekondari, mfumo unawakataa kwa sababu hawajasoma ualimu.

“Serikali ingetengeneza sera madhubuti ya kutusaidia sisi tunaotoka vyuoni, ili kama leo nikitaka kufundisha Kiswahili nisikutane na msururu wa masharti ya kujiajiri. Tukihitimu tutambulike na kusaidiwa ili tusimame,” anasema.

“Nina rafiki zangu wamesoma usimamizi wa biashara, saikolojia, masuala ya benki, wako tu mtaani kama mimi na wengine ni wamachinga Kariakoo. Naamini kuna jambo serikali yetu inapaswa kufanya ili tusikae mtaani kama hivi,” anashauri.

Pia anasema elimu ya kujitegemea na ujasiriamali inatakiwa ifundishwe kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu. Hii itatusadia sayansi na teknolojia isituathiri sana.

Mhitimu mwingine, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, anasema alihitimu UDSM mwaka 2021 na kupata GPA ya 4.0, lakini hajapata ajira ya kile alichosomea. Anasema amefanikiwa kuajiriwa kwenye moja ya migahawa jijini Dar es Salaam, anakopika na kuhudumia wateja, tofauti na alichosomea.

TATIZO KIMFUMO

Aliyekuwa Mhadhiri Mwandamizi UDSM, Dk. Donath Olomi, anasema wahitimu wa chuo kikuu na wa ngazi mbalimbali, kushindwa kujiajiri ni tatizo la kimfumo linalohitaji kurekebishwa.

“Mfumo wetu haujawa na kile kitu kinaitwa meritocracy (kutambua uwezo wa mtu). Mtu mwenye GPA kubwa hawapaswi kuwa wanazunguka barabarani. Mfumo ulipaswa kuwatambua na kuwawezesha,” anasema.

Dk. Olomi anasema mifumo ya ajira ilipaswa kuwatambua wahitimu wenye ufaulu wa juu na kuwapa kipaumbele, huku vyuoni na kwenye ngazi za elimu, zikiwafundisha na kuhakikisha wanafaulu kwa haki bila upendeleo.

“Mfumo wa ajira haujazingatia vizuri kuchagua watu wenye uwezo mkubwa. Hapa unazungumzia watu wachache wenye upekee.  Lakini tunaangalia pia maandalizi ya jumla kwa vijana wetu kuona fursa mbalimbali ndani na nje ya nchi,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Ushirika cha Wajasiriamali Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUGECO), Revocatus Kimario, anasema kuna pengo kubwa kati ya ujuzi unaotolewa chuoni na ule unaohitajika kwenye soko la ajira.

“Chuo ni kiwanda kinachozalisha bidhaa ambayo ni rasilimaliwatu, swali la kujiuliza ni je, tunazalisha kweli watu sahihi wanaohitajika sokoni? Wengi wanaotoka vyuo vikuu wana ujuzi pungufu,” anasema.

UELEWA WA CHINI

Kimario ambaye amekuwa akilea vijana kitaaluma na kuwatafutia ajira za muda nje ya nchi, anasema wahitimu wengi wana uelewa wa kawaida na wanakosa maarifa yanayohitajika kwenye soko la ajira.

“Kuna utafiti umetoka unaonesha kwamba asilimia 69 ya wahitimu hawana uwezo wa kuchambua kitu. Hili ni tatizo kubwa mno,” anasema.

Anasema vyuo vikuu vinakosa masomo ya ziada nje ya yale yaliyoainishwa kwenye kozi mahsusi, yanayoweza kumpa mhitimu maarifa yenye tija.

“Mwaka jana nilikuwa nina nafasi za kupeleka vijana 360 Ujerumani, tulishindwa kwa sababu vijana hawajui Kijerumani,” anabainisha. 

UDSM YAANIKA UKWELI

Naibu Makamu Mkuu wa UDSM (Taaluma), Prof. Bonaventure Rutinwa, anasema kila sekta nchini ina uhaba wa nguvu kazi na kinachokwamisha kuajiri ni fedha.

“Takwimu zinaonesha uhaba wa madaktari katika hospitali bingwa ni asilimia 70, lakini kuna madaktari 5,000 mtaani hawana ajira. Hapo huwezi kusema ni kwa sababu hawakuandaliwa vizuri, ni kwa sababu ya uwezo mdogo wa kuajiri na hii ndiyo changamoto kubwa hasa sekta ya umma,” anasema.

Anasema uhaba wa wafanyakazi uko katika sekta zote, akisema kwamba wapo pia walimu ambao hawana ajira, wakiwamo wa masomo ya sayansi.

Prof. Rutinwa anasema asilimia 80 ya soko la ajira nchini ni kampuni ndogo na za kati, ambazo zina uwezo wa kuajiri watu watatu hadi watano, wakati kila mwaka wanafunzi 100,000 wanahitimu vyuo vikuu, UDSM ikiwa na wahitimu 15,000 kwa mwaka.

 MABORESHO MITAALA

Prof. Rutinwa anasema chuo hicho kimeanza kufanya maboresho ya mitaala, ili kuongeza kiwango cha elimu ujuzi kwa wanafunzi.

“Mimi nimefundisha Kiswahili sekondari na baadhi ya wanafunzi wangu ni magwiji wa Kiswahili leo lakini sikuwa na cheti cha ualimu. Mambo mengine ni sera zetu. Hakuna mwalimu wa chuo kikuu mwenye cheti cha ualimu. Tatizo ni kwamba hata walimu wanahangaika,” anasema.

Anashauri kwamba kunapaswa kufanyika tathmini ya uhitaji wa soko la ajira, ili kupunguza mafuriko (idadi kubwa) ya wahitimu wasio na ajira.

Anasema vyuoni wanatoa ujuzi wa aina tatu, unaohusisha uwezo kujua na kung’amua mambo, kutenda na mtizamo wa kuendelea kujifunza.

Prof. Rutinwa anashauri wazazi na walezi, kuwajengea watoto maarifa hasa nidhamu ya kazi na kuheshimu muda, ili wanapokuwa watu wazima, waweze kushirikiana na jamii inayowazunguka.