Mbowe acharuka saruji kupanda bei

By Godfrey Mushi , Nipashe Jumapili
Published at 09:50 AM Jun 30 2024
Saruji yapanda bei.
Picha: Maktaba
Saruji yapanda bei.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kupanda kwa bei ya saruji katika maeneo mbalimbali nchini kunatokana na kodi iliyowekwa na serikali katika bidhaa hiyo ambayo ni kati ya Sh. 7,000 hadi 9,000.

Akizungumza na wananchi wa Matui, wilayani Kiteto, mkoani Manyara katika mwendelezo wa mikutano ya ‘Operesheni GF’, Mbowe alisema katika kila mfuko mmoja wa saruji, serikali inaweka kodi hiyo.

"Mfuko mmoja wa saruji watu wa Matui (Kiteto), mnanunua kwa shilingi ngapi? 20,000/- Kwa taarifa yenu, kwenye kila mfuko mmoja wa cement (saruji), serikali ya CCM inaweka kodi kati ya Sh.  7,000 na 9,000.

"Matokeo yake, ukienda kununua mfuko wa saruji Sh. 20,000 au Sh. 21,000, tayari umeshalipa kodi ya serikali ya CCM. Kila kitu mnachonunua kina kodi ya serikali.

Amewaeleza kwamba wakienda kununua mabati, muda wa maongezi katika simu, umeme, mafuta ya taa, mafuta ya kupikia, sabuni au soda kote kuna kodi.

Mbowe amesema bidhaa za vinywaji kama soda, kiwandani ni Sh. 270, lakini katika kila chupa moja ya soda serikali imeweka kodi Sh. 230, hivyo ikimfikia mwananchi haipungui Sh. 600.

"Ndugu zangu kama tuna shida ya elimu bora tuna shida wote, kama tuna shida ya maji, tuna shida wote. Kama tuna gharama za maisha, wote tuna gharama za maisha. Sasa unakuta wananchi wa Matui hawana maji, yuko hoi, hajitambui sawasawa," amesema.

Mbowe na Mwenyekiti wa CHADEMA, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, wanazunguka katika majimbo 35 ya mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga kwa wiki tatu mfululizo, wakiendesha Operesheni GF.