TAHARUKI ilizuka jana asubuhi baada ya jengo la ghorofa nne kuporomoka Kariakoo, jijini Dar es Salaam na hadi jioni aliyefariki dunia alikuwa mtu mmoja na wengine 40 kujeruhiwa.
Tukio hilo lilitokea kati ya Mtaa wa Congo na Mchikichi, baada ya jengo hilo lenye maduka ya biashara kuporomoka na kufukia watu na mali zilizokuwapo.
Mashuhuda wa tukio hilo, walisimulia waathirika walivyopitia nyakati ngumu wakipiga kelele kuomba kuokolewa baada ya kufukiwa na vifusi vya jengo hilo ambalo inadaiwa chini lilikuwa likijengwa.
Mmoja wa watu waliokuwa ndani ya jengo hilo, mama mwenye watoto wawili, alionekana akilia na kumwomba Mungu kuwanusuru na kifo. Baadhi walionekana wakiwapigia simu ndugu zao na wako walioongea nao kwa saa kadhaa na baadaye hawakupatikana tena.
HALI ILIVYOKUWA
Kasi ya uokoaji ilikuwa ndogo hadi ilipotimu saa 4:48 asubuhi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilipowasili na kuanza uokoaji ikiwamo kuwapelekea mitungi ya gesi watu waliokuwa chini ya ghorofa.
Ilipofika saa 6:30 mchana, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lilifika kuongeza nguvu za uokoaji, hali iliyoibua shangwe kutoka kwa wananchi ambao waliwapokea kwa kuwapigia makofi.
Baada ya kuporomoka kwa jengo hilo, shughuli mbalimbali sokoni hapo zilisimama kwa muda kati ya mitaa ya Mchikichi na Congo. Baadhi ya wataalamu walioongoza uokoaji ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi.
SHUHUDA MBALIMBALI
Wakala wa usafirishaji mizigo inayotoka China, Kabila Juma, alisimulia kuwa alishuhudia ghorofa hilo likiporomoka na halikuporomoka ghafla bali lilianza taratibu.
Alisema baadhi ya watu waliokuwa ndani ya jengo hilo wakati likiporomoka, walitoka na wale waliokuwa maduka ya chini, wengi wao walishindwa kutoka kwa wakati, hivyo mara moja walianza uokoaji.
Ally Salehe anayejishughulisha na ubebaji mizigo, alisema katika jengo hilo kulikuwa na ujenzi unaendelea kwenye maduka ya chini.
RAIS SAMIA
Kutokana na maafa hayo, Rais Samia Suluhu Hassan aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Idara ya Menejimenti ya Maafa kufanya kila linalowezekana kufanikisha uokoaji na tiba kwa majeruhi.
“Wakati hilo likiendelea na tunamwomba Mwenyezi Mungu awape pona ya haraka majeruhi. Tuwaombee pia utulivu na subira ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wenzetu wanaotafuta riziki zao katika eneo hili muhimu kibiashara nchini ambao kwa namna mbalimbali wameathiriwa na ajali hii,” alisema.
ATEMBELEA MAJERUHI
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, jana alifika eneo la tukio na baadaye kuwatembelea majeruhi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kuviagiza vyombo vyote vya usalama kuhakikisha watu wote waliokwama ndani ya jengo hilo wanaokolewa na mali zinalindwa.
Alisema katika ajali hiyo mtu mmoja ameripotiwa kufariki dunia hadi jana jioni na Muhimbili walikuwa wamepokea jumla ya majeruhi 40 ambapo kati yao, 33 walitibiwa na kuruhusiwa.
Katika eneo la tukio, Majaliwa alisema majeruhi wengine wamepelekwa Hospitali za Rufani za Mwananyamala, Amana na Temeke.
Alitumia fursa hiyo kuwahakikishia Watanzania kuwa kazi kubwa ya uokoaji inaendelea na vyombo vyote vya ulinzi na uokoaji vipo katika eneo hilo, hivyo amewataka waendelee kuwa na subra.
Majaliwa pia alimwelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dk. Jim Yonazi, kusimamia uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
“Wataalam mnaohusika na masuala ya ujenzi fanyeni ukaguzi wa ujenzi wa majengo unaoendelea,” aliagiza nakusisitiza kuwa kazi ya uokoaji itaendelea hadi kuhakikisha anatolewa hadi mtu wa mwisho.
“Nikiwa hapa nimeona mtu mmoja ametoka na amesema wenzake wapo chini,” alisema.
Pia aliagiza kwa wanaojenga majengo mapya katika eneo hilo kuhakikisha yanakuwa na ubora ili kuepuka matukio kama hayo kujitokeza tena.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema: “Nitoe rai kwamba muda huu si wa kulaumiana kwamba nani amesababisha hili tatizo. Ni muda wa kuokoa uhai wa wenzetu.”
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alisema jeshi hilo limetoa askari wa kutosha kuimarisha ulinzi na usalama wa mali za watu walioathirika na atakayebainika kuziiba atachukuliwa hatua.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Soko la Kariakoo, Martin Mbwana, alisema ni mapema kujua idadi ma maduka yaliyokuwapo ndani ya jengo hilo pamoja na mali zilizopotea.
AQRB WAELEZA KISHERIA
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Edwin Nnunduma, alisema sheria ya ujenzi inazuia jengo kutumika kabla halijakamilika.
“Ili jengo litumike, linapata vibali kutoka halmashauri. Tunajua lilikuwa linatumika huku linajengwa. Watu ambao wanaweza kutoa maelezo mazuri ni halmashauri. Hatujui lilikuwa likitumika katika hatua gani. Lingekuwa liko kwenye ujenzi, sisi tungekuwa tuna taarifa za nini kimetokea,” alisema.
Alisema bodi hiyo inatuma timu yake kuchunguza ili kubaini chanzo cha ajali hiyo na ndipo watatoa taarifa na ushauri wa kitaalamu kwa umma.
HAKI ZA WAATHIRIKA
Wakili wa Mahakama Kuu, Jebra Kambole, alisema waathirika wa ajali hiyo wanaweza kudai fidia kwa mmiliki.
“Kama mmiliki alitakiwa ahakikishe eneo lake lote linakuwa salama, kwa kuzingatia ubora wa jengo na kila kitu. Hii ni kanuni ya occupiers liability (mzigo kwa wamiliki) ambayo mmiliki wa eneo anawajibika moja kwa moja. Fidia haijaainishwa, inategemea na madhara aliyopata mtu,” alisema.
MATUKIO KAMA HAYO
Desemba 21, 2022, katika Kijiji cha Sembeti Marangu, mkoani Kilimanjaro, jengo la ghorofa ambalo ujenzi wake ulikuwa ukiendelea, liliporomoka na kusababisha vifo vya mafundi watano na majeruhi kadhaa.
Mwaka 2006 huko Chang’ombe, Dar es Salaam, jengo la Hoteli ya Chang’ombe Village (sasa Tanzania Hotel), liliporomoka na kuua watu wanne. Pia mwaka 2013, ghorofa lingine liliporomoka katika Mtaa wa Indira Gandhi, Dar es Salaam na kuua takriban watu 36, chanzo kikitajwa kuwa ujenzi usiozingatia utaalam.
Hadi gazeti hili linakwenda mtamboni shughuli za uokoaji zilikuwa zikiendelea maeneo hayo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED