Lissu awaangukia mawakili msaada walioenguliwa

By Waandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 07:17 AM Nov 24 2024
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Picha: Mtandao
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amewaomba mawakili nchini kusimama na kufungua mashauri yenye maslahi kwa umma kuwatetea wagombea wote walioenguliwa katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa bila kufuata vigezo vya kikanuni ili haki ichukue mkondo wake.

Lissu alitoa ombi hilo juzi jijini Mwanza katika mwendelezo wa ziara yake ya kuwanadi wagombea wa chama hicho katika nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa. 

Alisema kuwapatia msaada wa kisheria wote ambao wanahisi hawakutendewa haki wakati wa mchakato mzima wa kupata wagombea katika uchaguzi huo kinyume cha sheria na kanuni, kutasaidia hatua muhimu kuchukuliwa na kuwafanya wananchi kupata machaguo yao sahihi.  

Alitaja wakati huu kuwa si wa mawakili kuwa na upendeleo kwa chama chochote kile cha kisiasa bali kuonyesha ukakamavu na utumishi wao kwa jamii katika kusaidia upatikanaji wa haki kwa wale wote wanaodhani waliondolewa bila kufuata vigezo vya kikanuni. 

Lissu alisema chama hicho katika wilaya ya Nyamagana, kimesimamisha wagombea nafasi ya Mwenyekiti  165, walioenguliwa 11 huku wajumbe wakiwa 924 na walioenguliwa ni 24. Kwa wilaya ya Ilemela, alisema walisimamisha wagombea 131 nafasi ya mwenyekiti na kati yao, wanane walienguliwa huku nafasi ya wajumbe zikiwa na wagombea 694 na 10 wakienguliwa. 

“Ninaifahamu vizuri wilaya  hii ya  Tarime  kwa zaidi ya mika 20.  Nimeoa  huku, nimefanya kampeni na kina marehemu Chacha Wangwe.  Migogoro  ya Nyamongo ninaifahamu  sana. Tutahakikisha  tunatetea haki zenu ili kuipata Tarime Mpya,” alisema Lissu. 

Aidha aliwataka wanachama wa CHADEMA kujitokeza kwa wingi katika kipindi cha kampeni na wakati wa uchaguzi ili kuondoa malalamiko ya kupata viongozi wasiofaa baada ya kukamilika kwa uchaguzi. 

BITEKO APIGA KIJEMBE 

Wilayani Mbogwe mkoani Geita, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)  Dk. Doto Biteko amevikejeli vyama vya upinzani kuwa hakuna chenye nia ya kufanya kazi na kuwaletea maendeleo kama ilivyo CCM bali wanahitaji vyeo kwa ajili ya kujitambulishia kwenye misiba au kwenye harusi wakialikwa. 

“Hoja zetu Chama Cha Mapinduzi ni maendeleo yenu na kutaka kuondoa umasikini miongoni mwa watu na hili ndilo jambo ambalo tunaendelea kulisukuma. Nimekuja kuwaambIa hapa kuwa hakuna mtu atakayeshinda bila kupigiwa kura, hivyo kama mlivyoenda kujiandikisha, vivyo hivyo jitokezeni pia kupiga kura,” alisema Dk. Biteko ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. 

Pia alisema alisema chama hicho hakihitaji wala hakitajihusisha na ushindi wa kubebwa kwani wanahitaji ushindi halali kutoka kwenye sanduku la kura.

AHADI HUDUMA BORA

Wilayani Kahama, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya, Mussa Bukango, akinadi wagombea wa chama hicho alisema endapo wangombea wake watapata ridhaa ya kuongoza serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, watahakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi pasina kupokea fedha ya aina yoyote kama ilivyozoeleka.

Alisema, endapo atabainika kiongozi kutoka chama hicho akipokea fedha kutoka kwa wananchi wanaofika ofisini kupata huduma watamwajibisha kwa kumnyang’anya kadi ya uanachama na kukosa sifa, kwani viongozi wasiokuwa waadilifu wamekuwa wakitumia mwanya wa kuomba rushwa kwa wananchi ndipo wawahudumie hilo wao wanalipiga marufuku.

Kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa zinaendelea katika maeneo mbalimbali nchini ambako jana jioni wilayani Kahama mkoani Shinyanga Naibu Katibu Mkuu Zanzibar kutoka Chadema, Salum Mwalimu alifanya mkutano uliowakutanisha wananchi na wanachama wa chama hicho wilayani humo akiwanadi wagombea wa chama hicho.

Imeandaliwa na Vitus Audax, Remmy Moka (MWANZA), Shaban Njia (KAHAMA), Samson Chacha (TARIME).