Kampeni uchaguzi S/Mitaa zashika kasi

By Waandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 07:10 AM Nov 24 2024
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla.
Picha:CCM
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla.

KAMPENI za uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu, zimepamba moto huku vyama vinayoshiriki vikinadi sera na wagombea wao ili kushawishi wananchi kuwachagua.

Wakati kampeni hizo zikiendelea, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitacheka na mtu katika kushika dola huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kikidai kuwa chama tawala kinategemea vyombo vya dola  kuwakamata na kutaja sababu tano za kukiondoa madarakani CCM.

Aidha, Chama cha ACT Wazalendo jana kilimnadi mgombea wa CHADEMA na kueleza kuwa adui wa vyama vya upinzani ni chama tawala.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla, akiendelea na ziara yake ya kampeni mkoani Dar es Salaam, akiwa jimbo la Kibamba jana, alisema wamejipanga kuhakikisha wanashinda kwa kishindo.

“Katika uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa tutashinda na tunataka ushindi wa kishindo na kwa namna ambavyo CCM tumejipanga ni sawa na kusema yanayoendelea ni sawa na kusema yajayo yanafurahisha,” alisema.

Makalla alisema CCM inauchukulia uchaguzi huo kwa umuhimu mkubwa kwani inatambua kazi ya chama cha  siasa ni kushika dola na Chama hicho kinaanza na kushinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Kazi ya chama cha siasa kilichosajiliwa ni kuhakikisha kinashika dola maana kazi ya kuhubiri kwenda mbinguni hiyo inafanywa na viongozi wa dini.

1

“Kwa kutambua umuhimu wa kushika dola ndio maana katika uchaguzi huu CCM imeweka wagombea wake kwa asilimia 100, kwani hakuna mtaa, kijiji wala kitongoji ambacho tumeacha, kote tumesimamisha wagombea kwa nafasi zote,” alisema.

Alisema vyama vingine havina utayari ndio maana wameshindwa kusimamisha wagombea katika nafasi zote na mpaka sasa kuna mitaa ambayo tayari wagombea wake hawana washindani.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ipinda wilayani Kyela, Mbeya  aliwakumbusha wanachama wake kuhusu misingi minne muhimu inayosaidia chama hicho kuendelea kusimama imara na kushinda.

Aliwataka viongozi wake kusimamia haki kwa wote bila kujali itikadi za vyama vya kisiasa, aliongeza kuwa kila mwananchi anapaswa kuwa na uhuru wa kufanya shughuli zake kwa furaha na amani.

Alisema demokrasia inahitaji viongozi wachaguliwe kwa njia  ya kupigiwa kura na wanapaswa kuwa na hofu ya Mungu ili kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.

“CHADEMA bado ni chama imara licha ya fitina tunazokutana nazo. Tunapambana  hatukati tamaa. Ninatoa  pongezi kwa wananchi wa Ipinda na wagombea wao kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato huu kati ya vitongoji 30 vya mji huu,” alisema.

Alisema wamefanikiwa kusimamisha wagombea 27 akisema ni hatua kubwa kwao na kwenye vijiji na mitaa bado wamefanya vizuri.

Akirejelea  mafanikio ya kihistoria ya uchaguzi wa 2015 ambao walipata zaidi ya madiwani 1,200 na kushinda nafasi nyingi za ubunge, alithibitisha  nguvu ya chama hicho licha ya kukosa dola.

 Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi (Sugu), alisema ajenda kuu ya chama chao ni kukiondoa CCM madarakani akieleza kwamba kimeshindwa kutimiza matarajio ya wananchi.

 Alisema hali ya maisha imekuwa ngumu na serikali imeshindwa kutoa huduma bora za matibabu na kuhakikisha huduma za kijamii zinapatikana kwa bei nafuu,” alisema.

Sugu alitaja sababu tano za kuking’oa CCM madarakani kuwa ni viongozi wake kutochaguliwa kihalali, kushindwa kufanya vikao vya uwazi vya mapato na matumizi na kudai kimeuza huduma za mihuri ya vijiji.

Kadhalika alisema kutumia michango ya misiba kwa manufaa yao binafsi na kutumia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa upendeleo, huku wakikandamiza vyama vya upinzani kwa kutopewa mgao wa fedha hizo.

 ACT WAZALENDO

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, akihutubia wakazi wa kijiji cha Milola A, Kata ya Milola, jimbo la Mchinga mkoani Lindi, aliwataka wananchi kuchagua viongozi watakaoshirikiana nao kujiletea maendeleo akiwamo Abdallah Shedafa.

Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe, akiwa katika kijiji cha Bunyambo,  jimbo la Muhambwe, alisema wananchi wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji ambalo linaweza kutatuliwa kwa viongozi wa vijiji kukaa na mamlaka za maji, kuzitatua. Alisema CCM inapuuza changamoto ya maji inayowakabili wananchi.

Naibu Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara wa chama hicho, Julius Masabo, alimnadi mgombea wa uenyekiti wa CHADEMA, Marisiana Damasi, katika Kijiji cha Nyarugusu, Kata ya Kizazi, jimbo la Muhambwe na kusema adui wa upinzani ni CCM.

Alisema ACT Wazalendo, ilimnadi mgombea huyo kwa kuwa haijasimamisha mgombea kwenye nafasi ya uenyekiti kijijini hapo.

“Tushirikiane kuhakikisha tunaifuta CCM kwenye Kijiji chenu. Mpeni kura mama Merisiana na wajumbe wa ACT Wazalendo tuliowasimamisha,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita, akiwa katika kijiji cha Kiwalala, jimbo la Mtama, alisema CCM imevigeuza vijiji kuwa makazi ya maskini kwa kusimamia mapato na matumizi ya vijiji kwa usiri.

Aliwataka wananchi kuchagua wagombea wa chama hicho, ili wasimamie mapato kwa uwazi na kwa maendeleo ya wanakijiji wote.

·         Imeandikwa na Romana Mallya, Restuta James na Grace Mwakalinga.