Hatima kikokotoo kujulikana Mei Mosi

By Vitus Audax , Nipashe Jumapili
Published at 09:43 AM Apr 21 2024
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi.
PICHA: MAKTABA
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi.

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, amesema suala la kanuni mpya ya kikokotoo cha mafao ya wastaafu litajulikana Mei Mosi, Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Akijibu hoja mbalimbali za wabunge bungeni jijini Dodoma, Katambi amesema serikali haiwezi kufumbia macho wala masikio suala hilo.

Amesema licha ya maelezo mbalimbali yanayotolewa ndani na nje ya Bunge, suala hilo linatarajiwa kutolewa majibu na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi, yakakayofanyika jijini Arusha.

“Rais ameshatoa maelekezo zaidi ya mara mbili kwamba tulifanyie mapitio upya kuona namna ya kukifanyia maboresho zaidi ili wastaafu wasipate shida, tayari tumeanza kazi hiyo na sheria inatutaka kufanyia maboresho kila baada ya miaka mitatu na tayari imepita.

“Tunaendelea kulifanyia kazi maana tumepokea maelekezo ya Rais pamoja na Bunge, lakini pengine tunaweza kusikia kauli ya Rais katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, Siku ya Mei Mosi atakapokutana na wafanyakazi kueleza suala hili, hivyo tumelipa uzito unaostahili kuhakikisha tunaliweka sawa,” amesema.

ULIPAJI MISHAHARA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amesema wizara yake ipo katika mabadiliko makubwa yanayolenga kuwanufaisha na kuwainua watumishi wote katika nyanja mbalimbali.

Wakati akihitimisha hoja za wabunge na Bunge kuidhinishia wizara hiyo Sh. trilioni 1.10 kwa mwaka 2024/25, Simbachawene amesema kwa sasa hakutakuwa tena na malimbikizo ya mishahara, kwa kuwa fedha kwa ajili ya ulipaji zinatolewa kila mwaka.

Amesema kwa mwaka 2023/24, ilichukua fedha ya bajeti ya serikali ya Sh. bilioni 153.9 na kwa mwaka 2024/25 zimeombwa Sh. bilioni 150.8 na kuwa, hali itaendelea kwa utaratibu huo kila mwaka, kwa kuwa lengo la Rais Samia ni kila mtu apate anachostahili bila kudhulumiwa haki yake.

Pia, amesemaserikali inaendelea kulipa malimbikizo ya mishahara na watumishi 26,331 wamehakikishiwa kulipwa zaidi ya Sh. bilioni 39.55.

Kuhusu upandishaji vyeo, Simbachawene amesema serikali imerejesha utaratibu wa kupandisha vyeo watumishi kila baada ya miaka mitatu tofauti na awali ilikuwa ni baada ya miaka minne.

Amesema Rais Samia ameridhia kupandisha vyeo watumishi 81,515 waliokasimiwa katika bajeti ya mwaka 2023/24 kwa gharama ya Sh. bilioni 130.47.

Vilevile, serikali imepanga kuwapandisha vyeo watumishi 219,924 waliokasimiwa katika bajeti ya 2024/25, kwa gharama ya Sh. bilioni 252.7 na kufanya idadi hiyo kufikia 301,439, kwa miaka miwili ya fedha.

Amesema serikali imelipa mishahara kwa wafanyakazi wa mamlaka za serikali za mitaa 113 zenye jumla ya watumishi 691 kwa awamu.

Awamu ya kwanza, serikali imetenga Sh. bilioni 3.5 kwa ajili ya kugharamia mishahara ya watumishi 474 wa mamlaka za serikali za mitaa 101 ambazo zimebainika kuwa na uwezo mdogo kutokana na kushindwa kuwalipa.

“Nisisitize madeni ya watumishi hawa ambayo wanadai mamlaka hizo, ziwalipe na sisi tutaanza kuchukua hatua kwa wakurugenzi ambao tunapeleka maelekezo ya kulipa stahiki za madeni yanayotokana na watumishi walio chini yao halafu hawafanyi hivyo, hatua za kisheria tutazichukua kwa njia za kiutumishi,” amesema.

Amesema hiyo ni kutokana na kuwa kama mchezo, kwani watumishi wanalalamika maelekezo yanatolewa kwa mkurugenzi, lakini hawataki kuwalipa, hivyo kuahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Waziri Simbachawene amesema baadhi ya maeneo nchini yana upungufu wa watumishi, huku mengine yakiwa na watumishi wengi kupita kiasi, waking’ang’ania yenye mazingira mazuri na kuacha maeneo ya pembezoni.

Serikali imeamua baada ya majadiliano ya wizara tatu za Utumishi, TAMISEMI na Fedha, baada ya bajeti hiyo watahakikisha wanafanya mgawanyo wa walimu nchi nzima.

“Naomba niseme hapa, tusirudi tena hapa kulalamika kwa kuwa tutakapoanza operesheni hii haitamuacha mtu na wala haitakuwa na upendeleo, lakini tutazingatia hali na sababu mahususi walizonazo watumishi wetu,” amesema.

“Katika kutekeleza hili pia, lipo suala limeibuka la wenza na kwa kuwa mwajiri ni serikali na inahimiza maadili, hivyo tutahakikisha kila mwenye mwenza wake wa kweli wanakwenda kufanya kazi katika eneo moja hata kama siyo kituo kimoja,” amesisitiza.

UMILIKI NDEGE ATCL

Kuhusu kuhamisha umiliki wa ndege kutoka Wakala wa Ndege za Serikali Tanzania (TGFA) kwenda Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), amesema ni hoja inayoibuka mara kwa mara, lakini tayari limejadiliwa na utekelezaji unaendelea.

“Tunatambua kwa sasa ATCL inafanyakazi nzuri na tayari tulishakaa kamati kuhusu suala hili na utaratibu unaendelea, lakini tutambue kuhamisha ndege sio suala la haraka kiasi hicho, hivyo kuna michakato yake ya kimataifa na pia kitaifa inayoendelea,” amesema Simbachawene.

USAILI KIDIJITALI

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema tayari serikali imetatua kero ya watu kusafiri kutoka mikoani kwenda Dodoma kufanya usaili kwa ajili ya ajira mpya.

Amesema kutokana na malalamiko kuhusu watu wanaoomba fursa za ajira kulazimika kufunga safari na kutumia gharama kubwa kwenda Dodoma kufanya usaili, ufumbuzi wake umepatikana na sasa utafanyika kwa njia ya kijitali.

Pia, wizara hiyo imeanza usaili kidijitali kupita mfumo wa ‘Online Aptitude Test System’.

“Mara ya kwanza ulitumika kufanyia usaili Tanzania nzima na kwa siku hiyo, kwa mara ya kwanza hatukupata lalamiko lolote kuhusu utaratibu huu,” amesema Ridhiwani.

Amesema malengo ya serikali baada ya kuonekana kuwa umefanikiwa ni kuhakikisha taratibu nyingine za usaili katika kada zote unafanyika kupitia mfumo huo ili kufanyika maeneo yao.

“Nataka niwahakikishie sasa kwa wale wanaotoka katika mikoa ya mbali na Dodoma wakiwamo wa upande wa visiwani, sasa wataweza kufanya usaili wakiwa katika maeneo yao,” amesema.