CCM hatucheki na mtu katika kushika dola tumejipanga: Makalla

By Maulid Mmbaga , Nipashe Jumapili
Published at 08:42 AM Nov 24 2024
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla akizungumza na wanachama wa chama hicho.
Picha:Mpigapicha Wetu
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla akizungumza na wanachama wa chama hicho.

KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Amos Makalla amesema chama hicho hakicheki na mtu katika kushika dola na kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu wamejipanga kuhakikisha wanashinda kwa kishindo.

Makalla ameyasema hayo  jana akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kibamba jijini Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa mikutano yake ya kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka.

Amesema kuwa kwa sasa chama hicho kimeendelea kufanya kampeni za Uchaguzi huo na walizindua kampeni zao rasmi Novemba 20 mwaka huu katika mikoa yote nchini na tangu kuanza kampeni hizo wagombea wa Chama hicho wataibuka na ushindi wa kishindo .

"Katika uchaguzi huu wa Serikali ya Mitaa tutashinda na tunataka ushindi wa kishindo.Kwa jinsi ambavyo CCM tumejipanga  ni sawa na kusema yanayoendelea ni sawa na kusema yajayo yanafurahisha," amesema Makalla.

Akisisitiza zaidi amesema uchaguzi huo  ni muhimu na CCM inachukulia uchaguzi huo  kwa umuhimu mkubwa kwani inatambua kazi ya chama cha  siasa ni kushika dola na Chama hicho kinaanza na kushinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

"Kazi ya Chama cha siasa kilichosajiliwa ni kuhakikisha kinashika dola maana kazi ya kuhubiri kwenda mbinguni hiyo inafanywa na viongozi wa dini. Kwa kutambua umuhimu wa kushika dola ndio maana katika uchaguzi wa serikali za mitaa CCM imeweka wagombea wake kwa asilimia 100.

"Vyama vingine havina utayari  na ndio maana wameshindwa kusimamisha wagombea katika nafasi zote na mpaka sasa kuna Mitaa ambayo tayari wagombea wake hawana washindani,"amesma Makalla.

Pia amesema katika maeneo ambayo wapinzani hawajasimamisha  wagombea  kampeni ziendelee maana kutakuwa na ndio au hapana.