ACT - Wazalendo yalia na usikilizaji wa rufani

By Grace Mwakalinga , Nipashe Jumapili
Published at 10:16 AM Nov 17 2024
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Isihaka Mchinjita.
Picha:Mtandao
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Isihaka Mchinjita.

CHAMA cha ACT Wazalendo kimeeleza kusikitishwa na mwenendo wa usikilizwaji wa rufani za wagombea ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa.

Mchengerwa aliagiza utekelezaji wa agizo kufanyika kwa mapitio ya kuenguliwa kwa wagombea.

Kupitia taarifa ya chama hicho iliyotolewa jana,  Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Isihaka Mchinjita, alisema tathmini waliyofanya imebaini  kamati za rufani zimeendelea kuwaengua wagombea wao.

Alisema hata pale ambapo makosa yaliyojitokeza yalikuwa madogo, hayapaswi kuathiri mchakato wa uchaguzi.

Mchinjita alisema wagombea wao kutoka majimbo mbalimbali, yakiwamo Tandahimba (500) Newala Vijijini (93), Kinondoni (80) na Bukoba Vijijini (621) wameenguliwa licha ya maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mchengerwa, yanayotaka kuzingatia haki na kuepuka kuadhibu makosa madogo yaliyojitokeza.

Mchinjita alisema chama hicho kinalaani ucheleweshaji na kutochukuliwa hatua stahiki kwa wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo mengi kwa kushindwa kufanyia kazi maelekezo ya kuwasilisha fomu za uteuzi ili kufanya marekebisho kwa wagombea walioenguliwa.

Kutokana na hali hiyo, alisema wanamwomba waziri mwenye dhamana kusimamia utekelezaji wa agizo lake kwa kuhakikisha haki inatendeka.

“Tutamwandikia waziri orodha ya maeneo ambayo agizo lake halijatekelezwa kikamilifu pamoja na vielelezo husika.

“Tutachukua hatua za kisheria zikiwamo kufungua kesi mahakamani kupinga uamuzi wa kuwaengua wagombea wetu ili kuhakikisha uchaguzi unarudiwa katika maeneo husika,” alisema.