Mpango ang'aka madai ya rushwa kituo cha afya, aagiza uchunguzi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 02:08 PM Jul 14 2024
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.
Picha: Mpigapicha Wetu
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.

MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isack Mwakisu kutumia vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza malalamiko ya wajawazito kuombwa rushwa katika Kituo cha Afya Makere, Halmashauri ya Mji wa Kasulu.

Dk. Mpango alitoa maagizo hayo wakati akiwa katika Mji wa Makere baada ya kupokea malalamiko ya wananchi dhidi ya vitendo vya baadhi ya watumishi wa kituo hicho kuomba rushwa kwa wajawazito ili kuwapa huduma.

"Mkuu wa Wilaya una vyombo vinavyohusika na uchunguzi, hivyo unaposikia malalamiko ya wananchi elekeza vyombo vifanye uchunguzi ili uchukue hatua stahiki kwa watakaobainika, lakini msiwaonee," aliagiza Dk. Mpango.

Eva Moshi, mmoja wa wananchi waliopewa fursa  kuzungumzia changamoto zinazowakabili, alidai mjamzito anapokwenda kujifungua katika kituo hicho, kama hana Sh. 50,000 hatopata kadi ya kliniki na atajifungulia nje.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Zainab Katimba, alisema ofisi yake itachukua hatua za kinidhamu dhidi ya mtumishi yeyote atakayebainika kutoza mjamzito Sh. 50,000 kwa kisingizio cha kushindwa kufika kwa wakati katika kituo cha afya au zahanati.

"Kwa niaba ya Waziri Mohamed Mchengerwa, ninatoa maelekezo kwa watumishi wote wa kada ya afya kutimiza wajibu wao kikamilifu na kwa wale watakaoainika kuomba rushwa, hatua zitachukuliwa dhidi yao," alionya.

Mke wa Makamu wa Rais, Mama Mbonimpaye Mpango, alishukuru Naibu Waziri Zainab kwa kuahidi kutatua changamoto zinazokabili wananchi na kupongeza waliosema hadharani changamoto zinazowakabili ili zitatuliwe.

Dk. Mpango yuko katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma kukagua utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo.