Waziri asisitiza utafiti makusanyo ya kodi kwa biashara za mtandaoni

By Restuta James , Nipashe Jumapili
Published at 07:37 AM Nov 24 2024

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.
Picha:Mtandao
WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amekiagiza Chuo cha Kodi (ITA), kufanya utafiti maalum ili kubaini namna ya kukusanya kodi ya biashara za mtandaoni.

Katika taarifa yake iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, wakati wa mahafali ya 17 ya ITA, Dar es Salaam juzi, Dk. Nchemba alisisitiza dhamira ya serikali kuongeza wigo wa mapato kwa kuangalia uchumi unaoendelea wa kidijitali na kwamba kuna upotevu mkubwa wa mapato unaoikabili serikali, katika sekta za biashara za mtandaoni na kimataifa.

 "Tunatumai matokeo ya utafiti yatasaidia kupunguza ukwepaji wa kodi na kushughulikia mapungufu ya mapato yanayokabili serikali,” alisema.

Alisema serikali inaamini kwamba utafiti wa ITA, utatoa miongozo ya wazi ya kudhibiti biashara hizo kwa ufanisi.

Aliielekeza pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa wananchi ili kuongeza idadi ya walipakodi.

Aliwataka wahitimu wa ITA kuchangamkia fursa kwenye sekta za viwanda, biashara na madini, ili kujipatia kipato na kuchangia maendeleo ya nchi.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo, Prof. Henry Chalu, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau ili kufikia malengo ya nchi.

Prof. Chalu aliishauri sekta binafsi kuajiri wataalam wa kodi ili kurahisisha mchakato wa malipo na kupunguza makosa. 

Aidha, aliwataka wahitimu hao kufanya utafiti utakaoiwezesha TRA kuongeza idadi ya walipakodi, hivyo kuisaidia nchi.

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alikitaka chuo hicho kuja na mifumo bunifu ya kikodi, kutambua vyanzo vipya na kushughulikia mapungufu ya ukwepaji kodi.

Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Isaya Jairo, alieleza namna ITA imechangia kuimarisha mifumo ya kikodi nchini na Afrika, ikiwamo kuanzisha mamlaka ya mapato Sudan Kusini.

Katika mahafali hayo, wanafunzi 417 wa fani ya uwakala wa forodha, usimamizi wa forodha na kodi, kuanzia ngazi ya cheti hadi uzamili katika kodi walitunukiwa vyeti.

Alibainisha kuwa taasisi hiyo ni kitovu cha kuendeleza mifumo ya kodi, kwa kuchanganya maarifa ya nadharia na mafunzo kwa vitendo ili kukidhi matakwa ya taaluma.

 "Pamoja na uwezo wake thabiti wa mtaala na utafiti, ITA inasalia mstari wa mbele kushughulikia changamoto za kodi za Afrika," alisema.

Aliongeza kuwa maagizo ya Dk. Nchemba yanasisitiza jukumu muhimu la ITA katika kukabiliana na matatizo ya uchumi wa kidijitali.