WALIMU wa Shule ya Sekondari ya Jumuiya ya Wazazi (CCM) Meta, iliyoko katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, wamegoma kufundisha na kusimamia mitihani, kwa madai ya kutolipwa mishahara yao kwa zaidi ya miaka mitatu.
Wakizungumza na waandishi wa habari juzi walimu hao walisema, wamechoshwa na hali ngumu ya maisha inayowakabili kutokana na malimbikizo hayo, huku wakiitaka Jumuiya ya Wazazi ya CCM kuwalipa stahiki zao.
Mwalimu Seth Mwakilima, alisema wanashindwa kuelewa sababu ya hali hiyo, akidai sio wao tu, bali hata taasisi nyingine zinazomilikiwa na chama hicho hazijapatiwa stahiki zao.
Alisema wanachohitaji kwa sasa ni mishahara yao na fedha za kujikimu, si ahadi nyingine yoyote.
"Sisi walimu wa Shule ya Meta, tunahitaji kulipwa stahiki zetu, tumevumilia kwa muda mrefu, lakini sasa tumefikia mwisho.
Mwalimu Tabu Kahindi alisema maisha yao yamekuwa magumu ambapo kwenda kazini imekuwa ngumu zaidi kwa sababu ya kukosa nauli.
Alitolea mfano tukio alilokumbana nalo hivi karibuni ambapo aliumia akiwa kazini, lakini hajapata matibabu kwa sababu hana fedha za kutibiwa.
Mwalimu Tito Ngailo alisema hawana fedha za kulipa kodi wala ankara za maji na umeme, hali inayozidi kuwaweka katika mazingira magumu, huku familia zao zikitewagemea.
Mwalimu wa Taaluma shuleni hapo, Christopher Nswima, alisema hali ya kitaaluma kwa wanafunzi haikuwa mbaya hapo awali kwa sababu walijitahidi kufundisha kwa mshikamano.
Alisema ndani ya wiki hii, walimu walishindwa kuendelea kutokana na kuchoka kuvumilia hali ya kutolipwa mishahara, jambo ambalo limeanza kuathiri mitihani inayoendelea.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Lengai Akyoo, alikiri kuwapo kwa changamoto hiyo na kueleza hatua zilizochukuliwa kutafuta ufumbuzi.
Alisema suala hilo tayari limeripotiwa ngazi ya taifa, na timu imetumwa kushughulikia jambo hilo.
Alisema timu hiyo tayari ipo mkoani humo na itakapokamilisha kazi yake, itawasilisha ripoti kwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED