Wahamasishwa kujiunga katika vikundi kupata elimu ya biashara na mikopo

By Enock Charles , Nipashe Jumapili
Published at 09:55 AM Nov 10 2024
Fedha.
Picha:Mtandao
Fedha.

WANAWAKE wametakiwa kujiunga katika vikundi ili kupata elimu ya biashara na mikopo itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara Wauza Mazao Wanawake Sokoni Kariakoo (UWASOKA), Ashura Mhala aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wakihamasisha watu kujiunga na kikundi hicho.

Alisema kikundi hicho kimeundwa ili kukabiliana na changamoto za wanawake kiuchumi ikiwamo ukosefu wa elimu ya biashara na mikopo.

“Faida za kujiunga uanachama katika kikundi cha UWASOKA ni kujengeana uwezo katika mbinu za kufanya biashara kwa ufanisi ili kuwaongezea kipato na mitaji wanawake, lakini pia kuwaunganisha na wadau mbalimbali wa kibiashara.

“Kupitia kikundi hiki watapatiwa elimu hasa kuhusu biashara hii ya mazao ambayo ina changamoto zake na kama mtu asipozitambua mapema zinaweza kumgharimu, asitamani tena kufanya biashara katika maisha yake yote,” alisema.

Ashura alisema wanaojiunga hupata mikopo ya hadi Sh. milioni 15 kwa ajili ya kufanya biashara kwa urahisi zaidi tofauti na wale wanaokwenda kuiomba bila ushirikiano wa kikundi.

Alitaja faida nyingine ni kusimamia haki za wanawake katika biashara hasa yanapotokea majanga ya kibiashara ikiwamo biashara kuungua moto, utapeli na uporaji, unaoathiri zaidi wanawake kuliko wanaume kutokana na uwezo mdogo wa kujitetea.

“Yanapotokea majanga mbalimbali kama kuzuka moto na biashara kuungua, kuna mambo mengi huwa yanajitokeza ikiwamo biashara kusitishwa na baadaye kurudi upya katika maeneo ya biashara.

“Mara nyingine kwenye kuanza upya unaweza kukuta eneo lako limechukuliwa sasa kwa ushirikiano kupitia kikundi tunaweza kutetea haki zetu” alisema Ashura.