SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC), limetangaza ongezeko la safari za treni kwenda mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, na Arusha katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka.
Kwa miaka mingi, wakati wa msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, kumekuwa na mahitaji makubwa ya usafiri kwa mikoa hiyo. Kutokana na hali hiyo, TRC kwa miaka ya karibuni imekuwa ikiongeza safari za treni kwa abiria wanaokwenda na kutoka katika mikoa hiyo.
Kwa mantiki hiyo, TRC imesema hatua hiyo inalenga kukidhi mahitaji ya usafiri kwa abiria wengi wanaosafiri kuelekea Kaskazini Mashariki mwa Tanzania.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa TRC, Fredy Mwanjala, katika taarifa yake jana, alisema safari mpya ya treni itaongezwa siku ya Jumatano, hivyo kufanya jumla ya safari tatu kwa wiki kwenda na kutoka katika mikoa hiyo.
“Kuanzia Jumatatu mpaka mwanzoni mwa Januari 2025, treni zitakuwa zikibeba mabehewa 18 kwa safari moja, zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 1,000 na 1,200 kwa wakati mmoja,” alisema Mwanjala.
Alisema licha ya ongezeko la safari hizo, TRC haitakuwa na ongezeko la nauli katika kipindi hiki cha sikukuu, bali zitasalia kama zilivyo sasa.
“Safari za Moshi, nauli zitakuwa Sh. 16,500 kwa daraja la tatu, 23,000 kwa daraja la pili kukaa na 39,000 kwa daraja la pili kulala. Vilevile, kwa safari za Arusha, nauli zitakuwa Sh. 18,700 kwa daraja la tatu, Sh. 26,700 kwa daraja la pili kukaa na Sh. 44,400 kwa daraja la pili kulala,” alisema Mwanjala.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED