MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, ameihamasisha sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo wa kimataifa kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania.
Miongoni mwa fursa hizo ni uchumi wa buluu kwa faida za kiuchumi na hifadhi ya mazingira ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Dk. Mpango alitoa wito huo katika kotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Ashatu Kijaji, wakati akifungua mkutano wa kunadi fursa za uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu zilizoko Tanzania.
Mkutano huo ulioandaliwa na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Uchumi wa Buluu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ulifanyika pembezoni mwa Mkutano wa 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika mji wa Baku, Azerbaijan.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya, Shirika la Chakula Duniani (FAO), Shirika la Hifadhi ya Maliasili (IUCN) na mashirika mengineyo.
Dk. Mpango alisema ni muhimu kuwekeza katika shughuli endelevu za uchumi wa bluu na miradi ya kurejesha, kama vile marejesho ya mikoko, miamba ya matumbawe na bahari, uhifadhi wa maeneo ya mvua na kilimo cha mwani kinaweza kuongeza utenganishaji wa kaboni na kusaidia malengo ya kukabiliana na athari hasi za mabadiliko ya tabianchi kama ilivyoainishwa katika Itifaki ya Kyoto na Mkataba wa Paris.
Aliyataja maeneo ya uwekezaji kuwa ni pamoja na uchimbaji wa madini, uvunaji wa mafuta na gesi, ujenzi wa bandari kavu, uvuvi mkubwa katika kina cha Bahari katika eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 223,000.
Alisema uwekezaji huo utachangia kukuza uchumi wa nchi na wawekezaji, lakini pia utakuza ajira kwa makundi ya watu wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini na vyanzo vingine vya maji.
Dk. Mpango alibainisha kuwa Tanzania imeendelea kujenga miundombinu wezeshi ya kurahisisha ufanyajikazi katika sekta ya uchumi wa buluu ikiwemo kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya Bahari ili kuyaongezea thamani ikiwemo zao la mwani na kujenga viwanja vya ndege na bandari visiwani Zanzibar na mikoa ya kusini.
Wakizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe, na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Zahor Kassim El Kharousy, walieleza umuhimu wa uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu ikiwemo upatikanaji wa kodi pamoja na maendeleo ya watu.
Zaidi ya watu 200 toka mataifa mbalimbali wakiwamo viongozi waandamizi kutoka Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya, FAO, IUCN na mashirika mengine waliahidi kuendelea kusaidiana na Tanzania kwenye upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya masuala ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwenye sekta ya uvuvi Tanzania.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED