WAKATI dirisha dogo la usajili likikaribia, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, tayari amepenyeza faili la usajili akitaja maeneo anayotaka yaongezewe nguvu kwa ajili ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa wanayoshiriki, imefahamika.
Taarifa za ndani zimesema Fadlu ameweka wazi maeneo ambayo yanatakiwa kuboreshwa.
Akizungumza na Nipashe juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, kabla ya mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025), kati ya Tanzania dhidi ya Guinea, mmoja wa viongozi wa klabu hiyo alisema baada ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa pia kutakuwa na wachezaji watakaoachwa.
"Tayari kuna baadhi ya majina Fadlu amependekeza kusajiliwa, ametoa wasifu wa wachezaji hao, kazi imebaki kwa viongozi kumalizana nao ili Januari wawe sehemu ya kikosi chetu, lengo ni kuimarisha timu zaidi," alisema kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Aliongeza kwa sasa viongozi wanaanza mchakato wa kuzungumza na wachezaji hao ambao hata hivyo kiongozi huyo hakutaka kutaja majina yao.
"Muda ukifika mtawajua, lakini kocha ametaka kusajiliwa kiungo wa juu (kiungo mshambuliaji), beki wa kati na winga, tayari viongozi wameanza kufanyia kazi mapendekezo hayo, kwa sababu tunataka kuzidi kukijenga kikosi chetu," alisema kiongozi huyo.
Aliongeza kwa nafasi ya winga, kocha huyo ameridhishwa na uwezo wa Elie Mpanzu ambaye tayari ameanza mazoezi na timu hiyo ana atakuwa sehemu ya kikosi baada ya dirisha dogo kufunguliwa.
"Maeneo yaliyobaki ni kiungo kama nilivyosema na beki mmoja wa kati, hii Simba itakuwa tishio sana nawaambia, tusubiri muda utaongea," alisema kiongozi huo.
Wakati huo huo, Fadlu alikuwa ni sehemu ya viongozi na mashabiki walioshuhudia mechi kati ya Taifa Stars dhidi ya Guinea, ambayo ilimalizika kwa wenyeji kupata ushindi wa bao 1-0.
Katika mechi hiyo Fadlu amewatazama wachezaji wake watano waliokuwa sehemu ya vikosi vya timu hizo mbili katika mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi.
Nyota hao ni pamoja na Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein na Kibu Denis waliopeperusha bendera ya Stars huku pia Guinea kulikuwa na kipa, Moussa Camara.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED