Watiwa mbaroni wakidaiwa kubeba mafuta ya magendo

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:00 AM Jun 30 2024
Kamishna Msaidizi Moshi Sokoro.
Picha: Maktaba
Kamishna Msaidizi Moshi Sokoro.

JESHI la Polisi Kikosi cha Wanamaji limekamata majahazi mawili na watuhumiwa wanne wakiwa wamebeba mafuta ya kupikia madumu 1,731 yenye ujazo wa lita 20 kila moja wakidaiwa kuwa na nia ya kukwepa ushuru wa forodha.

Kamanda wa Kikosi hicho Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Moshi Sokoro, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, amesema majahazi hayo yamekamatwa kupitia ufuatiliaji maalum ulioanza mwezi Mei hadi Juni, 2024, ukilenga kudhibiti uhalifu ukanda wa Bahari ya Hindi.

Amesema majahazi yaliyokamatwa ni Mv. UKIMAINDI POA na jahazi lingine lisilokuwa na jina wala namba za usajili ambapo nahodha ni Masoud Rajabu.

"Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini watuhumiwa hao hawakuwa na nyaraka zinazothibitisha uhalali wa umiliki wa mizigo hiyo ya mafuta ya kupikia pamoja na nyaraka za usafirishaji," amesema.

Kamanda Sokoro pia amesema wamekamata faiba boti nane ambazo hazina usajili wala majina na zikiwa zinajihusisha na usafirishaji abiria kwa njia hatarishi katika fukwe za Kigamboni na Soko la Kimataifa la Samaki Feri.

Amesema Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa wafanyabiashara wasio waadilifu kuacha kusafirisha mizigo kwa njia ya bahari bila kuwa na nyaraka za mizigo hiyo.

"Wavuvi haramu na wamiliki wa boti pamoja na manahodha wanaobeba abiria kwa boti ambazo si salama maeneo ya Feri Kigamboni na Feri Magogoni, Jeshi la Polisi halitasita kuchua hatua kwa wahalifu wote wanaojihusisha na uhalifu huo," ameonya.

Kamanda Sokoro ameshukuru wananchi wanaochukia uhalifu na kuendelea kutoa taarifa za wahalifu kwao ili zifanyiwe kazi haraka na kuweza kutokomeza uhalifu kwa pamoja.