Watatu mbaroni tuhuma mauaji kada CCM

By Francis Godwin , Nipashe
Published at 11:48 AM Dec 17 2024
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi.

JESHI la Polisi mkoani Iringa linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Christina Kibiki.

Kada huyo aliuawa usiku wa kuamkia Novemba 13, mwaka huu, nyumbani kwake baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi, alisema baada ya kutokea kwa kifo hicho waliendesha operesheni na kuwakamata watu mbalimbali ambao waliwahoji.

Kamanda Bukumbi alisema wanaendelea na msako wa kuwakamata watuhumiwa wengine na kwamba kuna baadhi watawakamata muda wowote kuanzia sasa upelelezi utakapokamilika na kufikishwa mahakamani.

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wa kuwafichua wahalifu kwa kuwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi na wananchi utasaidia kupunguza uhalifu.

Katika tukio lingine, Kamanda Bukumbi alisema Jeshi la Polisi mkoani humo linamsaka askari polisi Rogers mwenye namba F.4987 wa Kituo cha Polisi Ipogolo, pamoja na askari wa Jeshi la Akiba, Thomas Mkembela kwa tuhuma za kumuua Nashon Kiyeyeu (23), mkazi wa Nyamhanga, Kata ya Kitwiru, Manispaa ya Iringa.

Kamanda Bukumbi alisema mauaji hayo yalitokea Desemba 14, mwaka huu, na Sajenti Rogers kwa kushirikiana na mgambo walimkamata mtuhumiwa huyo kwa kuiba simu na kumpiga hadi kupoteza fahamu.

Alisema kuwa Sajenti Rogers alipokea taarifa kutoka kwa mwananchi mmoja ambaye hakumtaja jina kuwa anamtuhumu Nashon Kiyeyeu kumwibia simu, ndipo aliposhirikiana na mgambo huyo kumkamata.

Kamanda Bukumbi alisema baada ya kumkamata wanadaiwa walimpiga mtuhumiwa huyo hadi kupoteza fahamu na kumpeleka katika hospitali binafsi na kisha Hospitali ya Rufani ya Iringa, lakini baadaye alifariki dunia.

Alisema baada ya tukio hilo, askari na mgambo huyo walikimbia kusikojulikana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linaendelea kuwasaka. 

Akizungumza na waandishi wa habari, baba wa marehemu, Lusia Kiyeyeu alisema alipata taarifa za kukamatwa kwa mtoto wake kutoka kwa dada yake alikokuwa anafanya kazi.

Alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo alifuatilia kituoni hapo, lakini hakumkuta kijana wake wala askari aliyemkamata.

Kiyeyeu alisema baadaye alienda Kituo Kikuu cha Polisi Iringa, lakini pia hakumkuta wala hakukuta jalada katika kituo hicho.