Wananchi watengeneza namba feki ili kuwahi matitabu ya bure Arusha

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 10:27 PM Jun 25 2024
Wananchi waliojitokeza kupatiwa matitabu ya bure Arusha.
Picha: Beatrice Shayo
Wananchi waliojitokeza kupatiwa matitabu ya bure Arusha.

MKUU wa mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ameshangazwa na kitendo cha baadhi ya wananchi kutengeneza namba feki ili kupatiwa matibabu kwa haraka.

Akizungumza na wananchi hao  waliojitokeza kwa ajili ya kupatiwa matibabu katika kliniki hiyo ya siku saba, Makonda amesema wapo ambao wamepatiwa namba juzi na bado hawajapatiwa huduma.

“Kuna watu wamejitengenezea namba zao jana wamekuja nazo leo badala ya wale waliobaki jana kuendelea na matibabu wakajikuta wamechukuliwa ambao ni wapya sasa tumekubaliana turejee kwenye namba zilizotolewa jana,” amesema Makonda huku wakimshangilia.

“Lengo ni kuhakikisha wale wote wa jana ambao wamepatiwa namba wamalizike katika matibabu alafu tuendelee na watu wa leo tumeelewana,”.

Aidha, amesema mpaka sasa madaktari na wauguzi wamefanya kazi kubwa idadi ya watu waliotibiwa imeenda mara tatu ya malengo waliyokusudiwa.

Makonda amesema kasi ya kuwahudumia wananchi imeongezeka na mapungufu ambayo yameonekana jana tayari wameyafanyika kazi.

“Madaktari wamefanya kazi kubwa wametoka majira ya saa 4 usiku na saa 11 alfajiri wapo katika hivi viwanja. Naomba niwahakikishie wananchi wote wa mkoa wa Arusha hakuna atakayekanyaga katika hivi viwanja asipatiwe matibabu,”amesema.