Walia kutolipwa fidia mradi wa bomba la mafuta

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 02:20 PM Jun 25 2024
Baadhi ya wananchi wanaodai hawajalipwa fidia kupisha mradi wa bomba la mafuta.
Picha: Maktaba
Baadhi ya wananchi wanaodai hawajalipwa fidia kupisha mradi wa bomba la mafuta.

BAADHI ya wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wameiomba serikali kuingilia kati na kuhakikisha wanafidiwa maeneo yao yaliyochukuliwa ili kupisha Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, Eliainaswa Elibariki, mkazi wa Zongomela na Christina Kasumbai, wamesema baadhi ya wananchi wameshalipwa fidia isipokuwa kuna baadhi hawajalipwa hadi sasa.

Amesema wao walipewa maeneo na serikali kwa lengo la kuyaendeleza katika shughuli mbalimbali ikiwamo kilimo, lakini mpaka sasa wamekosa fidia na badala yake wamepisha mradi ili wasije kuonekana ni kikwazo cha utekelezaji wake.

“Eneo lililopita bomba la mafuta ghafi tulipewa na Manispaa ya Kahama, wakati huo ikiwa Halmashauri ya Mji mwaka 2016 ili tuyaendeleze na tuliyaendeleza kwa kuweka misingi na kujenga nyumba, mwaka 2023 tuligundua tunapitiwa na mradi huo, lakini hakuna fidia yoyote tuliyopata," amesema Elibariki.

Hivyo, ameiomba serikali kuingilia kati na kuangalia namna ya kuwapatia fidia kama walivyofanya katika maeneo mengine kulipopita mradi huo.

Naye Christina Kasumbai, amesema baada ya kugundua eneo lake limepitiwa na mradi huo aliwatafuta wanaohusika kujua taratibu za kufuata ili apate kulipwa fidia, lakini hakuweza kupata majibu ya kuridhisha.

Hivyo, ameamua kwenda halmashauri na alipofika alipewa majibu kwamba eneo hilo tayari limeshalipwa fidia.

Akijibu hoja hiyo kwa njia ya simu, Ofisa Mawasiliano wa EACOP, Abbas Ibrahim, amesema eneo linalolalamikiwa linamilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, tayari waliishailipa halmashauri hiyo fidia kama waguswa wa mradi na siyo wao (wananchi) waliopewa eneo hilo kuliendeleza kama wanavyodai.

Katibu Tawala wa Wilaya Kahama, Hamad Mbega, amesema baada ya kupokea malalamiko hayo alilazimika kufuatilia ili kujua uhalali wa madai na kugundua kwamba eneo hilo tayari limelipwa fidia.

Amesema wameamua kukaa na Ofisi ya Mkurugenzi kujua namna gani wanaweza kutatua sambamba na kuwapatia maeneo mengine wakazi hao.