TMA yahadharisha hali mbaya ya hewa siku tano

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 09:15 AM Jun 25 2024
TMA yahadharisha hali mbaya ya hewa siku tano.
Picha: Maktaba
TMA yahadharisha hali mbaya ya hewa siku tano.

MAMLAKA ya hali ya hewa Tanzania (TMA) imetahadharisha wananchi katika mikoa mitano kuwapo kwa hali mbaya ya hewa kwa siku tano.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka hiyo imesema kutakuwa na upepo mkali unaosafiri kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara na Zanzibar.

Aidha, wananchi wanaofanya shughuli zao baharini wametakiwa kuchukua tahadhari kutokana na uwapo wa mawimbi makubwa na upepo mkali.

Mamlaka hiyo imesema hali hiyo mbaya ni ya siku tano kuanzia juzi Jumapili mpaka Alhamisi.

Imewatahadharisha watumiaji wa vyombo vya majini kuwa makini kutokana na hali hiyo mbaya ya hewa.

Aidha, shughuli mbalimbali za kiuchumi kama uvuvi na usafirishaji vitaathirika kwa kiasi kikubwa kwa siku hizo.