TCRA yaja na mkakati kuibua vinara kidijiti

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:36 AM Jun 25 2024
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir Bakari.
Picha: Maktaba
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir Bakari.

KATIKA harakati za kuhakikisha Tanzania inaandaa vinara wa kidijiti watakaokuwa na misingi imara ya kutatua changamoto na kuleta suluhisho za kuendesha shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo kidijiti, TCRA imekuja na mkakati imara wa kufikia malengo hayo.

Moja ya mikakati hiyo ni kuundwa na kuanzishwa kwa klabu za kidijiti kuanzia kwa wanafunzi wa ngazi ya awali hadi vyuo vikuu.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir Bakari, akielezea faida za klabu za kidijiti amesema ni nyenzo muhimu ya kuwakutanisha wanafunzi mbalimbali kujadili na kubadilishana uzoefu kwenye masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati (STEM) na TEHAMA.

Dk. Jabiri ameongeza kuwa vijana wanatakiwa watumie fursa hiyo ipasavyo kwa kuwa itasaidia kuipaisha nchi ya Tanzania kupitia uchumi wa kidijiti.

Baadhi ya wanufaika mbalimbali wa klabu hizo wakiwamo wanafunzi wa shule za msingi kutoka Unguja ambao ni Ibtisam Khalfan Abdallah (Skuli ya Turkish Maarif), Sarinah Salmin Sharif (Skuli ya Laureate), Zuhra Said Salum (Skuli ya Salim Turky) na Balqis Salum Khamis (Skuli ya Bububu), waliobuni mfumo wa kununua umeme na kuweka ankara za umeme kwenye mita za LUKU moja kwa moja, walisema wanawahamasisha wanafunzi wenzao kutumia fursa hiyo ipasavyo.

Wamesema itawawezesha kuja na mbinu mbalimbali za kuendesha nchi kidijiti na ni muhimu kufanya hivyo kwa kuwa uchumi wa sasa unaendeshwa kwa mapinduzi ya teknolojia.

Wanafunzi wengine wa shule za msingi kutoka Pemba ambao ni Hidaya Mohmed, Ahlam Ali (Michakaini A) Kauthar Mohmed (Al Khamis Camp) na Rayyan Masoud (Michakaini B), walisisitiza kuwa fursa hiyo kwao imekuwa muhimu na wanaahidi kuongeza vipaji vyao. 

Wamesema wameona matunda ya klabu za kidijiti ndani ya muda mfupi na baada ya kujiunga na klabu za kidijiti wameanza kupata matokeo chanya na mfano mzuri ni namna walivyofanikiwa kuja na suluhisho la kutoa elimu ya usalama mtandaoni.

Klabu za kidijiti hazikuishia tu shule za msingi, bali pia zilifika mpaka shule za sekondari, baadhi ya wanufaika wa klabu hizi kutoka shule ya sekondari Kijitonyama, Dar es Salaam ambao ni Tupokigwe Gwamaka, Keyline Mathias, Princess Wilfred, Ilham Suleiman, Rosemary Sanonga na Irene Basiga walielezea jinsi klabu ilivyowasaidia kubuni mradi unaohusisha michezo yenye manufaa kwa wasichana (Interactive ICT Career Exploration Game for girls).

Wanafunzi hao wamesema kuwa, wametambua umuhimu wa klabu hizo na kukiri kila kitu kinawezekana, hata Tanzania ya kidijiti inawezekana kwa kuanza na hatua muhimu kama hizo za kutengeneza klabu zinazosaidia kuwakutanisha, kubadilishana mawazo, kujadiliana na kufanya vitu vinavyohusiana na teknolojia hiyo.

Mkufunzi Msaidizi SUZA, Khailiya Masoud amesema TCRA imeona fursa madhubuti kwa kuanza na watoto wadogo katika kupandikiza mbegu za kidijiti.

Mpaka sasa klabu za kidijiti jumla zimezifikia taasisi 548 na wanafunzi waliofikiwa na klabu hizo wameonesha kupokea fursa hiyo na kuahidi kuifanyia kazi walete mageuzi kwenye utatuzi wa mambo mbalimbali ambayo mengi yanabebwa na kuwezeshwa na ubobevu wa TEHAMA ambao ndio msingi wa uendeshaji wa shughuli za kidijiti.