Samia, Rais wa Guinea Bissau wakubaliana kutoa fursa lukuki

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 04:39 AM Jun 23 2024
Rais, Samia Suluhu Hassan, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embalo (kushoto) Ikulu jijini Dar es Salaam jana.

RAIS Samia Suluhu Hassan na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embaló, wamejadiliana mambo mbalimbali yaliyojikita katika uchumi, uhusiano wa kikanda na kimataifa pamoja na ulinzi na usalama barani Afrika ili kukuza zaidi ushirikiano kati ya nchi zao.

Viongozi hao pia wameshuhudia utiaji saini Mkataba wa Mwongozo wa Ushirikiano baina ya nchi hizo uliofanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Januari Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa na Jamii wa Guinea-Bissau, Carlos Pinto Pereira.

Baada ya mazungumzo yao ya faragha Ikulu jijini Dar es Saalam jana, Rais Samia aliwaambia waandishi wa habari kuwa walijadili namna ya kukuza biashara, uwekezaji na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kilimo, hususani zao la korosho.

Rais Samia alisema walirejea adhma ya bara hilo ya kufungua eneo huru la biashara na kuhakikisha wanalitumia ipasavyo kwa kuanza kuchukua hatua za makusudi, ili kukuza biashara na uwekezaji kati yao kwa ushirikiano katika zao la korosho kwa kufanya utafiti na kuongeza thamani.

"Bara letu liko mbioni kuhakikisha Eneo Huru la Biashara Afrika linafunguka, lengo letu likiwa kukuza zaidi kiwango cha biashara kati ya nchi za Afrika. 

"Kuanzishwa soko hilo pia kutachochea ukuaji wa viwanda, uingizaji thamani wa mazao yetu pamoja na kuleta ajira kwa vijana wetu. Tumezungumza (Tanzania na Guinea-Bissau) mambo mengi yenye lengo la kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa yetu mawili. 

"Tulijikita zaidi katika nyanja za kiuchumi, pia tumebadilishana mawazo kuhusu masuala muhimu ya kikanda na kimataifa ikiwamo ukuzaji amani na usalama barani Afrika," Rais Samia alisema.

Mkuu wa Nchi alisema wamekubaliana pia kushirikiana na nchi zingine za Afrika kuhakikisha bidhaa za kilimo zinapata bei nzuri kwa kutengeneza umoja na kuwa na sauti katika soko la dunia.

Eneo lingine waliojadili ni namna watakavyoshirikiana kutumia fursa zinazopatikana katika uchumi wa bluu (uvuvi, utalii na ushafirishaji) kwa kuwa nchi hizo zina eneo kubwa la mwambao, hivyo kuwaweka katika nafasi nzuri ya kufanya biashara na nchi zinazowazunguka.

Vilevile, Rais Samia alisema wamekubaliana kuendelea kushauriana na kushirikiana katika kushughulikia changamoto mbalimbali za kiusalama barani, likiwamo tishio la ugaidi na biashara haramu ya dawa za kulevya.

"Ziara hii ni fursa kwa nchi zetu kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati yetu. Kama mnavyofahamu, mataifa yetu mawili yana uhusiano mzuri ambao umedumu kwa muda mrefu. Uhusiano kati ya watu wetu umedumu hata kabla ya nchi zetu hazijapata uhuru," Rais Samia alisema.

Aliitaja ziara ya mgeni wake huyo kuwa ya kihistora kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa Rais huyo kutembelea Tanzania na ni fursa muhimu katika kuimarisha uhusiano ulioanzishwa na Marais wa kwanza wa nchi hizo, Hayati Julius Nyerere wa Tanzania na Luís Severino de Almeida Cabral wa Guinea Bissau.

Rais Umaro Sissoco Embaló alisema nchi hizo zikifanya kazi kwa pamoja kubadilishana uzoefu, zitachangia kufikia ajenda ya Afrika Tunayoitaka 2063 - kuwa na amani ya kudumu, ustahimilivu wa kisiasa, kuleta maendeleo endelevu na kujenga mataifa yenye ustawi.

Alikaribisha Watanzania wanaojihusisha na sekta binafsi kutembelea nchi hiyo, ili kujifunza biashara katika nyanja mbalimbali. Nchi yake inaweza kuwa mlango wa kuingilia nchi zingine za Afrika Magharibi kupitia Mkataba ya Eneo Huru la Biashara la Afrika.

Alisema nchi hizo mbili zilishirikiana kuondoa ukoloni na ubaguzi, shughuli iliyofanywa na Kamati ya Ukombozi ua Umoja wa Afrika iliyokuwa na makazi yake Dar es Salaam.

Alisema mataifa ya Afrika yana jukumu muhimu kufanya kazi pamoja na kuandaa mustakabali wa dunia kwa kuwa yana rasilimali nzuri na uongozi sahihi unaoweza kuleta ustaarabu mpya.

Rais Umaro Sissoco Embaló yumo nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia juzi. Pamoja na mambo mengine, alitarajiwa kutembelea viwanda, Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Reli ya Kisasa (SGR).