Mwinyi akataa kuongezewa muda u-Rais

By Rahma Suleiman ,, Romana Mallya , Nipashe
Published at 10:04 AM Jun 25 2024
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha: Maktaba
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

SIKU moja baada ya mjadala kuhusu pendekezo la kuongezwa muda wa uongozi kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi kutoka miaka mitano hadi saba, mwenyewe amepinga na kusema ataongoza kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Taarifa iliyotoka Ikulu na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Charles Hilary, imesema kuwa Rais Mwinyi ataendelea kuheshimu utaratibu uliowekwa wa kuchaguliwa kila baada ya miaka mitano.

“Rais Dk. Mwinyi ni muumini wa kufuata Katiba na sheria za nchi, tunapenda kusisitiza kwamba maoni hayo kuhusu kuongezwa muda, sio ya rais wala sio ya Chama Cha Mapinduzi Zanzibar,” ilisema taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo ilisema maoni hayo pia yamekwenda mbali zaidi hata kutaka uchaguzi mkuu wa mwakani wa kumchagua rais wa Zanzibar usifanyike, jambo hilo halina tija wala faida kwa nchi na Chama Cha Mapinduzi chenye kufuata misingi ya demokrasia.

Taarifa hiyo, imewataka wananchi wenye mawazo tofauti na hayo wafunge mjadala huo.

Mjadala huo uliibuka baada ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Mohamed Said Dimwa, kusema Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya CCM, Zanzibar wamepitisha pendekezo la kuishauri kamati maalum kuridhia kuongeza muda wa Rais wa Zanzibar kuongoza nchi katika muhula wake kwanza kwa kipindi cha miaka saba badala ya mitano.

CCM: HAKUNA MPANGO KUMWONGEZEA MUDA 

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA Amos Makalla, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendeshwa kwa vikao na hakuna mpango wa kumwongezea muda wa kuongoza nchi, Rais Mwinyi.

Katika mahojiano maalum na Globaltv yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam, Makalla alipoulizwa kuhusu suala la Zanzibar, alisema juzi na jana alilisikia jambo hilo na kuona kwenye vyombo vya habari.

“Niseme mimi ni Katibu wa Uenezi CCM, mimi ndiye ninayesema mambo yote ya chama katika vikao, mimi ninaingia katika Sekterarieti, ninaingia Kamati Kuu, ninaingia Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu.

“Chama chetu kinaendeshwa na vikao kwa hiyo sijaona kikao chochote ambacho kitanifanya mimi nishindwe kuelewa uwapo wa jambo hilo.

“Niseme tu taarifa zinazosambaa hazipo katika utaratibu wa vikao vya chama chetu na nilivyosoma nimeelewa kwamba ni mawazo, lakini hata kile kikao cha Zanzibar ambayo ni Kamati Maalum Mwenyekiti wake anakuwa Makamu Mwenyekiti na Rais wa Zanzibar, nako halijafika kwa hiyo mawazo ni mawazo,” alisisitiza Makalla.

Hata hivyo, Makalla aliomba anukuliwe; “mimi kama msemaji wa chama, chama chetu kinaendeshwa kwa vikao na taarifa hiyo sina na mpango huo haupo. Aliwaomba Watanzania kuwa hilo jambo halipo na kwamba, Chama Cha Mapinduzi kinaheshimu utawala wa sheria.

“Tunajua kuna Katiba na ukisoma Katiba ya Zanzibar Ibara 28(2) (i) kinaeleza kwamba, Rais wa Zanziabr atakaa miaka mitano na baada ya hapo kutakuwa na uchaguzi vivyo hivyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Makalla alisema ili kuthibitisha hilo wametoka kujadili suala la bajeti na tayari serikali imewasilisha bajeti ikiwamo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani.

“Kwa hiyo haiwezekani kukawa na jambo hilo wakati suala hilo tayari lipo kwenye bajeti na kila chama kinajiandaa na harakati zake kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu. Kwa hiyo niwatoe hofu Watanzania, mawazo yanaruhusiwa yamesemwa ni mawazo, lakini hayajapita katika vikao rasmi vya Chama Cha Mapinduzi,” alisisitiza.

Dk. Dimwa alisema uamuzi huo wa kumwongezea muda Rais Mwinyi wa kuongoza nchi unatokana na kuridhishwa na kasi yake ya kiutendaji katika kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 kwa zaidi ya asilimia 100 ndani ya kipindi cha miaka mitatu na miezi kadhaa toka aingie madarakani.

Katika maelezo yake, Dk. Dimwa alisema kuwa CCM Zanzibar imeona serikali kuingiza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ni hasara na matumizi mabaya ya fedha za walipakodi kwa kuwa wananchi wanahitaji maendeleo endelevu na Rais Dk. Mwinyi anafaa kuongezewa muda, ili Zanzibar iwe nchi ya visiwa iliyoendelea kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Awali, akizungumzia kuhusu ajenda na hoja ambazo huibuka kuelekea Uchaguzi Mkuu, Makalla alisema siku zote lengo la chama cha siasa ni kushika dola na kamwe hakihubiri kwenda mbinguni.

“Dola inaanza na kushinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa ndio maana umetuona tumekuwa kwenye ziara ndefu ya mikoa 11 kuhamasisha viongozi wa ngazi zote kujiandaa na uchaguzi na mwakani, tukishinda vizuri tutashinda kwa kishindo,” alisema.

Makalla alisema ndani ya CCM wanajiona wako salama, wako imara na kauli yao ni umoja ni ushindi.

Alisema walipopita katika mikoa walichokiona ni uhai wa chama upo vizuri na wanaona watashinda kwa kishindo katika uchaguzi huo.

Tofauti na wenzao, alisema wameona uchaguzi wao wa ndani haujawaacha salama, kumekuwa na makundi, mgawanyiko wa viongozi mbalimbali wakati CCM uchaguzi ukiisha wanahakikisha hauleti makundi na wanapotoka nje wanakuwa wa moja.