Musoma Vijijini wajipanga kuwa na shule za kidato cha tano, sita

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 05:06 PM Jul 04 2024
Baadhi ya wanafunzi wakifunza masomo kwa vitendo, katika moja ya sekondari jimboni humo.
Picha: Sabato Kasika
Baadhi ya wanafunzi wakifunza masomo kwa vitendo, katika moja ya sekondari jimboni humo.

JIMBO la Musoma Vijijini mkaoni Mara, limo katika harakati za kuandaa wataalam wa fani mbalimbali wa baadaye kwa kutenga baadhi ya sekondari kuwa na kidato cha tano na sita kwa masomo ya sayansi.

Kwa mujibu wa mbunge wa Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo, sekondari hizo ni Suguti ambayo itakuwa na mchepuo wa  PCM, PCB, CBG na EGM, Mugango itakayokuwa na CBG na EGM.

"Tumeanza kupata usajili wa "High Schools za masomo ya sayansi. Sekondari hizo kila moja ina maabara tatu za masomo ya sayansi, bweni moja au mawili, maji na umeme," Prof. Muhongo amesema.

Lakini pia amesema, ipo Kasoma Sekondari, ambayo ni kongwe, yenye Kidato cha tano na sita ikiwa na masomo ya HKL, HGK, HGL, na kwamba imeongezewa HGF na HGL.

Mbunge huyo amesema, vijana wa Tanzania, wakiwamo wa Musoma Vijijini wanapaswa kutayarishwa kuingia kwenye ushindani wa ulimwengu wa sasa na ujao wa ajira, taaluma, ubunifu na uchumi.

"Maoteo au global forecast,  ifikapo mwaka 2030, ni kwamba utakuwapo upungufu wa wataalamu milioni 80 ifikapo mwishoni mwa mwaka huo, kampuni kubwa duniani zitatumia takribani Dola za KImarekani trilioni 3.2, kila mwaka kuwekeza kwenye Artificial (AI)," amesema.

Amesema, kampuni zitafanya hivyo, ili kutatua tatizo la ukosefu wa wafanyakazi duniani, na kwamba roboti zitatumika kwa wingi, na kufafanua kuwa ni muhimu kuwekeza katika masomo ya sayansi.

"Tunataka kuanza na sekondari chache, lakini zinahitajika nyingi zaidi. Kwa mfano sekondari za Bugwema, Nyakatende, Kiriba na Etaro ambayo ina chamba cha kompyuta, zote zina maabara tatu," amesema.

Mbali na hizo, mbunge huyo amezitaja sekondari nyingine zinazofaa kuwa na kidato cha tano na sita kuwa ni Rusoli, Makojo na  Nyambono, ambazo amesema kila moja ina maabara mbili.

"Wanavijiji wanaowamba wadau  elimu wakiwamo wazaliwa wa Musoma Vijijini waishio maeneo mbalimbali nchini, waendelee ushirikiana na serikali kuchangia ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi kwenye sekondari za jimboni humo," amesema.