Miundombinu wezeshi urejelezaji Kumaliza tatizo la taka nchini

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 06:50 PM Jul 04 2024
Mkurugenzi wa Taasis ya Nipe Fagio, Anna Rocha.

IMEELEZWA kuwa Tanzania inaweza kudhibiti na kufikia adhima ya taka sifuri kwa kunua magari makubwa, urejelezaji na kuweka miundombinu wezesheji kwa uchakataji taka.

Hayo yameelezwa leo mkoani Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi Inayojihusisha na Udhibiti wa Taka Nchini  ya Nipe Fagio, Anna Rocha  katika Mkutano wa Kimataifa wa Miji ya Taka Sifuri uliowakutanisha wadau wa nchi mbalimbali duniani ulioandaliwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na Mtandao wa Vikundi vya Wananchi GAIA.

Amesema kwa sasa Tanzania imeanza kufanya vizuri katika udhibiti wa taka kutokana na baadhi ya mikoa kuanza kutekeleza mfumo wa taka sifuri. 

Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni pamoja na Arusha, Dar es Salaam, Tanga na Zanzibar akisisitiza lengo la mkutano huo ni kujadiliana na kupeana elimu na namna ya kuifikisha katika mikoa mingine.

Amesema katika mkutano huo wawakilishi kutoka mikoa mingine nchini walikubali kupeleka elimu hiyo katika maeneo yao ili kushirikiana kwa pamoja kudhibiti taka Kama ilivyokuwa kwa Zanzibar amabao wamefanikiwa kupitia mfumo huo.

Amesema mfumo wa taka sifuri utasaidia kuifanya nchi kuwa safi, kuongeza ajira kwa vijana, kupata kipato kupitia faida zitakazo patikana kutokana na urejelezaji ikiwamo kuuza mbolea na chakula cha kuku.  

Mathalan kwa Tanzania, amesema wakati wanaanza na mfumo taka sifuri walitathmini uhalisia wa mazingira na maisha ya Watanzania ambayo ilitoa jawabu la mifumo gani ibuniwe kulingana na uhalisia wa maisha ya Tanzania na hali yake kiuchumi, ili kudhibiti taka.

"Kupitia hiyo tumeweza na hivi sasa Tanzania ni moja ya nchi zinazofanya vizuri Afrika kwa udhibiti wa taka," amesema Anna.

Katika maelezo yake, amesema msingi wa juhudi zote hizo ni kuhakikisha Tanzania na dunia kwa ujumla inakuwa mahali pazuri pa kuishi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Zanzibar, Mahmoud Mussa amesema utekelezaji wa mpango wa taka sifuri visiwani humo unalenga kuviweka safi visiwa hivyo.

Mzizi wa uamuzi huo ni kile alichoeleza, tangu Rais Hussein Mwinyi anaingia madarakani aliweka wazi kutoridhishwa na hali ya uchafu ndani ya Mji.
"Ile ilikuwa ni kauli mbiu kuhakikisha tunakwenda tunafika hatua tunaondoa tatizo la uchaguzi Zanzibar," amesema.

Ili kufanikisha hilo, amesema alikutana na wadau mbalimbali wenye uelewa na uzoefu wa Mfumo huo na kuwakutanisha na vijana wake ili waelimishwe namna ya kuutekeleza.

Naye Mratibu  wa Miradi ya Ufadhiri Kutoka Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini nchini (TARURA), Humphrey Kanyenye ameisihi jamii kushiriki na kuhusika kufikia malengo ya taka sifuri.

"Tunauwezo wa kupunguza taka kwa kutumia vikundi mbalimbali vilivyopo kwenye jamii zetu kwa kukusanya, kuchakata na kupata mbolea inayoweza kutumika katika kilimo, viwavi kwa ajili ya chakula cha kuku hivyo sisi kama TAMISEMI na TARURA wenye Miradi inayoendelea hasa katika Mkoa wa Dar es salaam ujuzi huu umetuongezea faida nyingine," amesema Kanyenye.

Amesema kupitia Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP) wameanza na Nipe Fagio na kwamba mpango waliona kwa sasa ni kuanzisha mfumo wa usimamizi wa taka ngumu. 

"Hii njia wanayoitumia wenzetu wa mataifa mengine ni nzuri, na itatusaidia sana kutokana na elimu ambayo imetolewa pale Bonyokwa ni mfano mkubwa, wananchi wanakusanya taka na kuzigawa katika mafungu matatu kisha wanazilejeleza na zinazosalia wanazipeleka dampo" amesema

Mfumo wa taka sifuri unajumuisha kuzigawa taka katika makundi manne, ambayo ni ya zile zinazooza, rejeshi, hatarishi na nyinginezo na kisha zinachakatwa na kurejelezwa kwaajili ya kupata bidhaa mbalimbali kama vile mbolea, chakula cha kuku pamoja na kupunguza mlundikano wa taka dampo.