Halmashauri Handeni watakiwa kutenga fedha kulipa madeni

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 07:29 PM Jun 22 2024
MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Dk. Batilda Buriani

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Dk. Batilda Buriani ameiagiza Halmashauri ya Handeni vijijini kuhakikisha inatenga fedha ili kuweza kulipa madeni ya Shilingi Bilioni 2.3 inayodaiwa na watumishi pamoja na wazabuni jambo ambalo limechangia kuongezeka kwa hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali.

Dk. Buriani ametoa maelekezo hayo jana wakati akiwa kwenye kikao cha baraza maalum la kupokea taarifa za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo halmashauri hiyo ilipata hati inayoridhisha ikiwa ni mwaka wa tano mfululizo.

"Pamoja na hati safi tuliyoipata na pamoja na kujibu hoja kuna mambo ambayo yametusababishia halmashauri yetu kuwa na hoja hizi nyingi ambayo yako ndani ya uwezo wetu na tukikubaliana kwa pamoja tunaweza kuyapunguza"

" Kwa mfano madeni ya watumishi Handeni ni halmashauri pekee kushinda halmashauri zote yenye madeni mengi ya watumishi na wazabuni lakini pia hata ule utayari wa kulipa hauonekani na fedha mnayotenga kulipa, mna madeni ya bilion 2.306 na fedha mnayotenga ni milion 24 hii tunaona kama ni takrima , tunaelekeza mtenge fedha za kulipa madeni ya watumishi na wazabuni haipendezi hawa watu wanakwenda mpaka kwa waziri Mkuu kudai madeni jambo hili mkalisimamie" alisisitiza Dk. Buriani.

Sambamba na hilo mkuu huyo wa mkoa ameitaka halmashauri kulipa deni la kiasi cha shilingi Million 17 ambalo linadaiwa na watumishi wastaafu katika halmashauri hiyo ambapo ameelekeza kabla ya kufika Juni 30 deni hilo liwe limeshalipwa.

"Watumishi wastaafu wanadai shilingi million 17 hili ni Deni la kufuta kabisa tuhakikishe kabla ya kufika Juni 30, 2024 hili deni la watumishi wastaafu liwe limefutwa kuna mambo mengine ambayo ni lazima tuyasimamie na kuuatekeleza wenyewe" alisema.