Watu kadhaa wahofiwa kufariki dunia Kenya

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:35 PM Jun 25 2024
Maandamano ya kupinga mswada tata wa fedha yafanyika katika sehemu nyingi nchini Kenya.
Picha: Maktaba
Maandamano ya kupinga mswada tata wa fedha yafanyika katika sehemu nyingi nchini Kenya.

WATU kadhaa wanahofiwa kufariki dunia huko nchini Kenya, kufuatia maandamano yanayoendelea nchini humo, yaliyolenga kupinga muswada wa fedha wa mwaka 2024.

Umati wa waandamanaji umejitokeza na kukusanyika katika barabara mbalimbali huku Polisi wakiwarushia mabomu ya machozi waandamanaji waliokuwa wamejihami.

Makumi kwa maelfu ya Wakenya wamekuwa wakiandamana mjini Nairobi tangu asubuhi ya leo, huku maandamano sawia yakifanyika katika miji na majiji mengine kote nchini.

Video kwenye mitandao ya kijamii inaonekana kuonesha maelfu ya watu wakitembea kuelekea mji mkuu kujiunga na maandamano, ambayo yaliitishwa kupinga msururu wa mapendekezo ya ushuru mpya katika Muswada wa Fedha.

Bunge la nchini Kenya hii leo limepitisha marekebisho ya muswada wa fedha kwa mwaka 2024.

Muswada huo wa Sheria ya Fedha wenye utata umepitia Kamati ya Bunge zima, ambapo wabunge walikuwa wakipiga kura ya marekebisho ya Muswada huo, sasa unasomwa kwa Mara ya Tatu.

Hii ni baada ya Wabunge 195 kupiga kura kupitisha muswada huo huku 106 wakipiga kura kukataa sheria iliyopendekezwa.

Makabiliano makali yamezuka katikati ya mji wa Nairobi baada ya polisi kuwatawanya waandamanaji wakipinga muswada wa fedha wa 2024.