Netanyahu: Vita Gaza karibuni kumalizika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:10 PM Jun 25 2024
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Picha: Maktaba
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

WAZIRI Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amebainisha kwamba vita vya kutumia silaha vinavyoendeshwa na jeshi la taifa hilo dhidi ya wapiganaji wa Hamas katika mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, viko karibuni kumalizika.

Netanyahu aliyaeleza hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na chombo kimoja cha habari cha Israel, ambako kwa mara ya kwanza tangu vita hivyo vianze ameonyesha matumaini ya kumaliza vita hivyo vilivyodumu kwa zaidi ya miezi saba.

“Hii haimaanishi kwamba vita vinakaribia kuisha, lakini vita katika awamu yake ya vurugu vinakaribia kumalizika huko Rafah,” alisema.

“Tukimaliza vita na Hamas mjini Rafah tunaelekea Lebanon, tutapeleka baadhi ya vikosi vyetu kuelekea kaskazini, na tutafanya hivyo kwa madhumuni ya kujihami, lakini pia kurejesha wakazi waliofukuzwa kwenye makazi yao.” 

Netanyahu pia alisisitiza kwamba hatakubali makubaliano yoyote ya muda, na kwamba lengo ni kurejesha mateka na kuangusha utawala wa Hamas huko Ukanda wa Gaza.

Akijibu swali kuhusu hatima ya Gaza baada ya vita, Netanyahu alieleza kuwa Israel itakuwa na jukumu la kutekeleza kwa muda kupitia udhibiti wa kijeshi.

"Pia tunataka kuanzisha utawala wa kiraia, kwa ushirikiano na Wapalestina wa ndani ikiwezekana, na pengine kwa usaidizi wa nje kutoka nchi za kanda, ili kusimamia misaada ya kibinadamu na baadaye masuala ya kiraia katika Ukanda wa Gaza," alisema.

BBC