Makabiliano washambuliaji na jeshi Urusi yaua 19

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:19 PM Jun 25 2024
Mmoja ya wafanyakazi wa dharura kwenye Sinagogi lililoshambuliwa huko katika jimbo la Dagestan, Urusi.
Picha: Gyanzhevy Gadzhibalayev/TASS/dpa/picture alliance
Mmoja ya wafanyakazi wa dharura kwenye Sinagogi lililoshambuliwa huko katika jimbo la Dagestan, Urusi.

RUSSIA imesema makabiliano yaliyokuwa yakiendelea kati ya jeshi la nchi hiyo na washambuliaji yamemalizika huku yakisababisha vifo kwa Warussia 19, kati yao maofisa wa polisi wakiwa 15 na wananchi wa kawaida wanne.

Inaelezwa kuwa juzi usiku washambuliaji hao waliokuwa na silaha walivamia makanisa ya Orthodox na Sinagogi katika mji mkuu wa Dagestan, Derbent na katika kituo cha ukaguzi cha polisi, huku kamati ya kupambana na ugaidi katika taifa hilo ikibainisha kuwa washambuliaji watano wameangamizwa.

Ilielezwa kuwa haijabainika kwamba kuna washambuliaji wengine waliotoroka, huku sababu ya mashambulizi hayo ikiwa bado haijajulikana.

Msururu huu wa mashambulizi yanayoelezewa kama ya kigaidi na mamlaka ya Russia yanakuja miezi mitatu baada ya shambulio lililodaiwa kutekelezwa na kundi la wanajihadi la Islamic State (IS) lililofanywa katika ukumbi wa Crocus City, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 140.

Aidha, ilielezwa kuwa Dagestan, eneo la Russia lenye waislamu wengi jirani na Chechnya, lilikuwa eneo la mapigano ya mara kwa mara na wanajihadi katika miaka ya 2000, kama sehemu kubwa ya Caucasus. Na kwamba uasi huo ulikomeshwa na majeshi ya Urusi baada ya miaka mingi ya mapigano.

RFI