WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo amesema bidhaa nyingi za Tanzania zimeshindwa kuingia kwenye soko la Marekani (AGOA) kutokana na kushindwa kukidhi vigezo na masharti yaliyowekwa kwenye soko hilo.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za ubora kwa kampuni na wajasiriamali mbalimbali zilizoratibiwa na Shirika la Viwango (TBS).
Kwenye tuzo hizo TBS ilishirikana na Mmalaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake (TWCC), SIDO, Chemba ya wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS) na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
Alisema serikali ya Marekani ilitoa fursa hiyo kama mkakati wake wa kuzikuza nchi za Afrika lakini baadhi ya nchi hizo ikiwemo Tanzania zimeshindwa kuuza bidhaa nyingi kwenye soko hilo.
Aliwataka wajasiriamali na wazalishaji nchini kuzalisha bidhaa zenye ubora ambazo zitaweza kuingia kwenye masoko makubwa ya kimataifa kama AGOA, Afrika Mashariki na kati na hata soko la ndani.
“Mataifa yote yaliyoendelea duniani huwa yanategemea soko la ndani kwanza sisi tuko milioni 62 kwa hiyo kama mtazalisha bidhaa ambazo watanzania watazipenda soko la ndani tu linaweza kuwasaidia,”alisema
Alisema tuzo hizo zimeonyesha umuhimu mkubwa hasa kutokana na washiriki wake kuongezeka kutoka washiriki 36 wa mwaka jana hadi kufikia washiriki 54 wa mwaka huu.
“Pamoja na haya lazima tufahamu kuwa bidhaa zozote zitaweza kushindana kwenye masoko kama mtaendelea kuzingatia ubora nawashukuru TBS mmekuwa kielelezo cha ubora,” alisema na kuongeza
“Kwa bara la Afrika TBS imekuwa mshindi wa taasisiz a ubora barani Afrika kwa hiyo inatambulika kuwa namba moja kwa masuala ya udhibiti na tuzo zinasaidia sana kuongeza thamani ya bidhaa za kampuni na wajasiriamali wanaoshinda,” alisema
Aliwataka watanzania kuwaunga mkono wenzao wanaozalisha bidhaa mbalimbali kwa kununua bidhaa hizo na kuachana na kasumba ya kuona bidhaa za nje kama bora zaidi ya zile zinazozalishwa ndani.
Aliwataka watanzania kupitia Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO), kuimarisha biashara zao kwa kupata mafunzo yanayotolewa na shirika hilo na baadaye kupewa nembo ya ubora bure na TBS.
Alisema idadi ya vijana wanaomaliza vyuo vikuu ni kubwa na serikali haina uwezo wa kuwaajiri wote hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuleta sekta binafsi ili iwaajiri vijana hao au wajiajiri wenyewe wakihitimu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo hizo, Cresensia Mbunda, alisema kila mwaka Wizara ya Vianda na Biashara kupitia TBS na ZBS wakishirikiana na sekta binafsi wamekuwa wakiandaa tuzo za ubora.
Alisema wanafanya hivyo kama sehemu ya kuhamasisha matumizi ya viwango vya ubora na ushindani katika sekta mbalimbali nchini na kutambua na kuthamini juhudi za wazalishaji waliofanya vizuri kwa mwaka.
Alisema timu ya majaji saba kutoka sekta binafsi na serikali walipitia na kuchakataa maombi 52 yaliyokusanywa kwenye kuwania tuzo hizo bila upendeleo wowote na kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED