Kampuni ya Madini za Geita Gold Mine Limited na Twiga Minerals Corporation zimetawala katika tuzo maalum za Usiku wa Madini kwa kufanya vizuri katika Sekta ya Madini na kujinyakuliwa tuzo mbalimbali.
Katika hafla hiyo iliyofana usiku wa Novemba 20, 2024, washindi wa Tuzo za Usiku wa Madini 2024 walitangazwa na kupatiwa tuzo maalum ikiwa ni sehemu ya kutambua michango yao katika ukuaji wa Sekta sambamba mchango wa sekta ya madini nchini Tanzania.
Mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Madini na Uchumi wa Buluu wa Kenya, Ali Hassan Joho, ambaye aliongozana na Waziri wa Madini wa Tanzania, Anthony Mavunde, pamoja na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Madini kutoka Uganda, Phiona Nyamutoro huku wadau wengine wa sekta ya madini kutoka ndani na nje ya nchi pia wakihudhuria tukio hilo lililobeba uzito mkubwa katika kuhamasisha uwajibikaji, uvumbuzi, na maendeleo endelevu ya sekta hiyo.
TUZO ZA CSR, MAZINGIRA, NA USALAMA
Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) na Shanta Mining Company Limited zilitunukiwa tuzo ya “Utendaji Bora Katika kipengele cha Wajibu wa Kampuni kwa Kijamii (CSR)” kutokana na juhudi zao za kusaidia maendeleo ya jamii zinazozunguka migodi yao kupitia miradi ya elimu, afya, na uboreshaji wa miundombinu.
Kwa upande wa “Utendaji Bora Katika Masuala ya Mazingira na Usalama,” washindi walikuwa Kampuni ya GGML, Shanta Mining Company Limited (New Luika), na IrasaNilo Gold Mine, ambao wameonyesha viwango vya juu vya uwajibikaji wa kimazingira na kuhakikisha usalama wa wafanyakazi na jamii.
TWIGA BARRICK YAIBUKA MSHINDI WA JUMLA
Twiga Minerals Corporation Barrick ilitangazwa kama mshindi wa jumla kutokana na mchango wake mkubwa katika nyanja mbalimbali, ikiwemo utendaji bora kwenye uwekezaji wa ndani, Kampuni hiyo ya ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick pia ilishinda tuzo ya “Utendaji Bora Katika Uwekezaji wa Ndani” kwa wamiliki wa leseni maalum za uchimbaji, ikijidhihirisha kama mfano wa kuigwa katika kukuza Sekta ya Madini nchini.
Kampuni hiyo pia ilijinyakulia Tuzo ya “Mdhamini Bora” katika Mkutano wa mwaka huu (2024), sambamba na tuzo ya “Maonesho Bora” kwa maonesho bora yaliyovutia na kuelimisha wadau wengi wanaohudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini 2024.
MCHANGO WA MAPATO KWA SERIKALI
Tuzo ya “Mchango Mkubwa kwa Mapato ya Serikali” ilikuwa na washindi kadhaa waliotambuliwa kwa mchango wao wa kifedha kupitia kodi na ada mbalimbali, washindi hawa ni pamoja na IrasaNilo Gold Mine, 21st Century Textile Ltd (kwa madini ya vito), Lemianatha Kabigumila (kwa madini mengine ya chuma), na Jitegemee Holdings Co. Ltd (kwa madini ya ujenzi, viwanda, na nishati). Aidha, washindi wengine katika kipengele hiki walikuwa Sakisa and Co. Ltd (kwa madini ya thamani), Sana Gems Ltd (kwa almasi), Tramic Industrial Material Resources (kwa vito visivyo safishwa), na Mineral Access System (Tanzania) Ltd (kwa madini mengine ya chuma).
UONGEZAJI THAMANI NA WANAWAKE
The Tanzanite Experience (Tanzania) Ltd ilitunukiwa tuzo ya “Utendaji Bora Katika Shughuli za Uongezaji Thamani” kutokana na ubunifu wake katika usindikaji wa vito vya thamani na mauzo yake kimataifa.
Kwa upande wa kutambua nafasi ya wanawake, Leminatha Kabigumila alishinda tuzo ya “Mwanamke Bora Katika Sekta ya Madini,” ikiwa ni mwaka wa pili mfulilizo kwake kushinda tuzo hiyo, ikiwa ni sehemu ya motisha wanawake wengine kushiriki zaidi katika Sekta ya Madini.
MZALISHAJI BORA WA NDANI WA MADINI MKAKATI
Mchimbaji mzawa Godlisten Mwanga alitunukiwa tuzo ya “Mzalishaji Bora wa Ndani wa Madini Muhimu ya Ndani” kwa juhudi zake katika uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite).
Kwa ujumla, lengo la Tuzo za Usiku wa Madini 2024 ni kutambua juhudi na mafanikio makubwa ya washindi wote katika kuchangia maendeleo ya sekta ya madini na uchumi wa Tanzania.
Lakini pia hafla hiyo ni sehemu ya Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini 2024 ulioanza Novemba 19 na unatarajiwa kuhitimishwa leo Novemba 21 2024.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED