WAKAZI wa Kata ya Malolo Tarafa ya Mikumi Wilayani Kilosa mkoani Morogoro, wamemkataa Hakimu wa eneo hilo kwa kile wanachodai kuwa ni amekaa muda mrefu huku akionesha kupenda rushwa.
Akijibu tuhuma hizo Mbunge wa Mikumi, Denis Londo alikiri kutokuwepo kwa sheria inayoruhusu kiongozi yoyote kukaa muda mrefu sehemu moja.
Wakazi hao wamesema hayo mbele ya Mbunge wa Jimbo la Mikumi Wilayani Kilosa, Denis Londo, alipofika katika kata hiyo kukabdhi gari la wagonjwa ili kunusuru vifo vya watu hasa wajawazito na watoto wachanga wanapokwenda kupata huduma.
Mmoja wa wakazi wa Malolo, Mgonela Kibiki anasema akiwa mkazi wa muda mrefu kwenye kata hiyo anashangazwa na Serikali kuendelea kumbakiza Hakimu huyo aliyekaa kwa zaidi ya miaka 25 kwenye kata hiyo na hivyo kujenga mazoea na kutokuwa mtendaji mzuri wa kazi zake.
Mgonela anasema ni vyema hakimu huyo akahamishwa kwa sababu anashindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo ambapo yeye aliwahi kupeleka kesi yake ya madai na mdaiwa kutakiwa kuwasilisha fedha kwa hakimu ili yeye akachukue na hakimu huyo kutomlipa zaidi ya shilingi milioni moja licha ya kuwa tayari amepokea.
Mbunge Londo aliahidi kulifikisha suala hilo kwenye vyombo husika ili liweze kufanyiwa kazi mara moja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED