RAIS Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi kutokupuuzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, watumie fursa hiyo kugombea na kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo, kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Samia ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi mkoani Mwanza, akielekea Geita kwa ajili ya kufunga maonesho ya teknolojia ya madini.
Alisema, ili kufanikisha hatua hiyo, inabidi wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, pamoja na lile la serikali za mitaa hususani wale ambao tayari wamefikisha umri wa miaka 18.
Alisema anatarajia kurejea mkoani humo, kushiriki na Watanzania kuadhimisha Kilele cha Mbio za Mwenge Kitaifa, kitakachofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba Oktoba 14, mwaka huu, yakitanguliwa na kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“Kilele cha mbio za Mwenge kitaifa kinatimiza miaka 60 ikiambatana na miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kuanzishwa kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi vyote kwa pamoja vimejenga historia ya kutimiza miaka 60 mwaka huu,” alisema.
Alisema ifikapo Novemba 27, mwaka huu, ni siku ya kupiga kura ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa na vitongoji, hivyo kila mwananchi anatakiwa kujitokeza kutekeleza haki yake ya msingi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, wakati akitoa salamu kwa niaba ya wananchi wake, alisema serikali ilitoa zaidi ya Sh. trilioni tano kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati iliyoko mkoani humo.
Aliwaomba wananchi mkoani hapa kujitokeza kwa wingi katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa , kwani mkoa umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo.
Wakati huo huo, vyama vya siasa visivyopata ruzuku serikali vimeomba kupatiwa, ili kushiriki uchaguzi kama vilivyowezeshwa mwaka 1995.
Wamesema ni muhimu kutafuta utaratibu, ili kuwezeshwa kushiriki katika uchaguzi huo muhimu.
Kauli hiyo iliyolewa jana, jijini Dodoma, mara baada ya kumaliza mkutano wa dharura wa Baraza la Vyama vya Siasa ambapo washiriki walipatiwa mafunzo kuelekea uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, alisema kuna vyama 19 vilivyosajiliwa, lakini si vyote vina uwezo wa kushiriki katika uchaguzi kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha.
“Tumekubaliwa hapa kuwa ni muhimu kutafuta utaratibu vyama viweze kuwezeshwa kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” alisema.
Alisema wameomba Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), iwapatie orodha ya vijiji, vitongoji na mitaa, kwa kila chama na iwekwe katika tovuti ya kila halmashauri.
Alisema kama TAMISEMI itazingatia maoni yao kutakuwa na uchaguzi bora na kuomba yasijirudie yaliyotokea katika uchaguzi kama huo, uliofanyika mwaka 2019.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini, alisema ni muhimu ikatolewa ruzuku kusaidia gharama za uchaguzi, ili kuongeza ushindani.
“Chama tawala hakiwezi kufanya uchaguzi peke yake, ni muhimu vyama vingine navyo viwafikie wananchi, ili kuwahamasisha, kuweka mawakala, mihuri na gharama nyingine,” alisema.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mrema, alisema uchaguzi ni gharama na vyama havina fedha, hivyo serikali iweke utaratibu wa kuhakikisha vinashiriki uchaguzi kama ilivyofanyika mwaka 1995 ambako wagombea wote waligharamiwa na serikali.
“Hoja hii tumeijadili haijapata majibu, lakini imechukuliwa, tunategemea itapata majibu baadaye. Nimetoa tahadhari kwa serikali kwamba, ina wajibu wa kuhakikisha vyama vyote vinashiriki uchaguzi , kwa kuwa ukiviachia vyama vijiendeshe vyenyewe nani anawajibika kutafuta fedha za uchaguzi katika chama peke yake?,”
“Vipo vyama vichache vinapata ruzuku kidogo, lakini kuna vyama vingi havipati hata hiyo ruzuku, ukitegemea vikashindane kwa usawa, tunakuwa hatutendi haki,” alisema.
Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, alisema: “Mambo makubwa matatu ambayo tunaamini TAMISEMI watafanyia kazi ni suala la uapishaji mawakala, tumejenga hoja ni vizuri waapishwe ngazi za vijiji, badala ya utaratibu uliotumika hivi sasa katika ngazi ya halmashauri, kwamba wakusanywe ngazi ya kata au halmashauri husika,” alisema.
Akifungua mafunzo hayo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alivitaka vyama hivyo kutotumia lugha za matusi, kashfa, uchochezi au vitendo vitakavyovuruga amani katika uchaguzi huo.
Alisema vyama vinapaswa kufanya siasa za kistaarabu wakati wa kampeni za kuwanadi wagombea wao.
“Lengo la mafunzo haya ni kuwakumbusha kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika kipindi mtakapokuwa mnajinadi kwa wananchim, ili kuwashawishi waamini na hatimaye kuwachagua wawakilishi kutoka katika vyama vyenu.
“Kuna maisha baada ya uchaguzi, hivyo tusije kudhani kila kitu kwetu ni uchaguzi pekee, amani na umoja wa taifa ni muhimu zaidi kuliko hata huo uchaguzi. Amani ikikosekana hata fursa tutakayopata ya kushiriki uchaguzi haitakuwapo,” alisema.
IMEANDALIWA na Remmy Moka (MWANZA) na Augusta Njoji (DODOMA)
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED