MKUU wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha leo Oktoba 6,2024, amezima jaribio la kumtorosha mtoto mwenye umri wa miaka 13 aliyeachishwa masomo yake kwa ajili ya kwenda Dar es Salaam kutumikishwa.
Utoroshaji huo umefanywa na mawakala ambao walimdanganya mtoto huyo kuwa wanampeleka kwa shangazi yake.
Amesema baada ya kupata taarifa basi alilopakiwa mtoto huyo liliamriwa kwenda kituo cha polisi na kisha kumteremsha mtoto huyo.
“Nilipata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya kitendo cha mtoto mdogo kusafirishwa kutoka Ngara mpaka Kahama kwa kutumia watu wanaosafirisha watoto kwa kusema wanaenda kufanya kazi, watu hawa wanajiita mawakala,” amesema Chacha.
Aidha, amesema baada ya mazungumzo naye alisema anatokea Ngara na waliokuwa wanamsafirisha walimlaghai kwamba wanampeleka kwa shangazi yake Kahama.
Amesema baada ya kufika Kahama akafaulishwa kwenye gari ambayo inaelekea Dar es Salaam ambako baada ya mtoto huyo kuona amepishwa eneo alipotaka kwenda akaanza kulia ndani ya basi hivyo baadhi ya abiria wasamalia wema wakatoa taarifa na gari hilo kutakiwa kwenda polisi ili kujiridhisha.
“Kwahiyo ndugu zangu abiria mtatusamehe sana kwa kuwasumbua na kuwaleteni kituoni hapa lengo letu lilikuwa ni jema na pengine ninyi msinge kubali kuona mtoto anasafirishwa kwenda kufanyishwa kazi, lakini tofauti na kazi pengine kuna mambo mengine wanawafanyia ambayo sisi hatuyajuhuhi,”RC Chacha amewatangazia abiria.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED