MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema Chama cha Wanasheria Zanzibar, kinapaswa kuwa kimbilio la wananchi pale haki zao zinapovunjwa.
Pia amesema chama hicho kinapaswa kuwa msatari wa mbele katika kupaza sauti za wananchi na kuwatetea.
Othman aliyasema hayo jana katika Hoteli ya Verde, Maruhubi mjini Zanzibar, alipofungua mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wanasheria Zanzibar, ambao pamoja na mambo mengine, utafanyika uchaguzi wa viongozi mbalimbali wa taasisi hiyo.
Alisema jumuiya hiyo ina wajibu, mbali na kupaza sauti haki za wananchi zinapovunjwa, kuchukua hatua stahiki kwa wanaohusika na uvunjaji wa haki hizo.
Makamu wa Kwanza wa Rais alisema chama hicho kinapaswa kuwa mlinzi namba moja wa Katiba ya nchi na mfumo wa utoaji haki, utawala wa sheria pamoja na demomkrasia.
Aliwaambia wanasheria hao kuwa wana wajibu wa kulinda haki za kiraia, kwa kuwa kazi mojawapo waliyo nayo ni kusimamia mashauri yenye maslahi na umma.
Kwa mujibu wa Othman, haipendezi pale haki za kiraia zinapokuwa hatarini ama kutokana na sababu ya wenye mamlaka au maslahi ya kibiashara, hivyo chama hicho kisikae kimya badala yake kitimize wajibu wake wa kupaza sauti kuutetea umma.
Alitoa wito kwa wanasheria kuendelea kujifunza, ili kukuza uwezo na ufanisi kwa kukabiliana vyema na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, kiuchumi na hata mwingiliano wa kijamii pamoja na matukio ya kihalifu ambayo hayakuzoelekea kusikika nchini.
Pia aliwataka wananasheria hao kutumia nafasi waliyo nayo katika kuchangia jitihada za kueleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia ushauri wao wa kisheria sambamba na kuhakikisha makubaliano na mikataba inazingatia vyema sheria, ili kuepuka migogoro.
Kuhusu uchumi wa Buluu, Othman alisema kuna fursa nyingi ikiwamo sekta ya mafuta na gesi asilia, sambamba na kulitumia vyema eneo la usafiri na usafirishaji wa anga, kwa kufuatilia fursa nyingi zilizoko na kujifunza ili kufaidika nao.
Aliwakumbusha wanasheria hao kuwa waadilifu wenye kufuata maadili ya taaluma na wananchi wapate fursa za kutumia haki zao bila vizuizi.
Waziri Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, alisema jumuiya hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa serikali na kwamba serikali itaendelea kujenga ushirikiano na taasisi hiyo.
Naye Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar anayemaliza muda, Masoud Rukazibwa, alisema chama kinakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwamo upungufu wa rasilimali hususan katika maeneo ya vijijini ambako huduma bado zinahitajika sana.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED