WANANCHI wenye hasira kali wa eneo la Kwa Mrombo, mkoani Arusha, jana Oktoba 12,2024 wamevunja nyumba na kuchukua kila kitu, ikiwamo matofali na kuacha eneo hilo bila chochote cha mtuhumiwa Jaina Mchomvu wa mauaji ya binti Mariam Juma (12).
Mwandishi wa habari hizi alivyofika eneo hilo aliona wananchi wakibomoa nyumba ya mtuhumiwa huyo na kuchukua kila kitu baada ya kumkosa.
Wananchi hao walichukua walichukua mabati ya nyumba hiyo baada ya kuiangusha chini na wengine walibeba matofali ya nyumba hiyo na kuacha eneo hilo likiwa jeupe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishana Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP, Justine Masejo, amesema tukio hilo lilitokea Oktoba 12, 2024 baada ya mwili wa mtoto huyo kukutwa chini ya uvungu wa kitanda ndani ya nyumba ya mtuhumiwa huku ukiwa na majeraha ya kukatwa na kitu chenye ncha kali
"Mtoto huyu alikuwa ametumwa dukani toka asubuhi lakini hakurejea na ilipofika mchana wazazi wake walianza kumtafuata maeneo mbalimbali baada ya kuingiwa na wasiwasi,"amesema
Masejo amesema hadi sasa wanawashikilia Jaina Mchomvu ambaye ni mama mwenye nyumba ambayo ndani ulikutwa mwili wa mtoto huyo, ambaye alikamatwa na Polisi huko Mabogini Moshi, mkoani Kilimanjaro alikokimbilia kujificha baada ya tukio hilo kubainika.
Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Arusha kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Aidha, alisema kuwa baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa Jaina Mchomvu, alihojiwa na kukiri kutenda tukio hilo la mauaji ya mtoto huyo na kwamba wanaendelea na uchunguzi.
Wakizungumza eneo la tukio mmoja wa wakazi wa eneo hilo,Juma Abdallah amesema jirani yao alianza kumtafuta mwanaye kuanzia asubuhi baada ya kumtuma vocha dukani bila kurudi.
"Lakini mchana alisikika mtoto mdogo kwenye nyumba inayodaiwa kumuua Mariamu akisema ameona mkono kwenye beseni na watu tulipokwenda tukaona mtoto huyu amekatwa katwa na kuwekwa kwenye beseni lililowekwa uvunguji mwa kitanda cha huyu mtuhumiwa,"amesema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED