ARSENAL mara nyingi imekuwa na nguvu ya kuvutia inayohitajika kusajili wanasoka wenye vipaji na wa kutumainiwa zaidi duniani, lakini wachezaji wake wengi wa kustaajabisha wamekuja wakati wa dirisha la majira ya joto.
'Washikabunduki' hao hawajawahi kuwa na matumizi makubwa ya fedha kwa usajili wa Januari na rekodi yao katika soko la majira hayo ya baridi ni mchanganyiko.
Wachezaji wachache wakubwa walisajiliwa Kaskazini mwa London Januari, lakini kumekuwa na hadithi kadhaa za mafanikio zinazojulikana na za mabadiliko.
Makala haya inaangalia usajili bora wa muda wote wa Arsenal katika kipindi cha Januari tangu dirisha hilo la majira ya baridi lilipoanzishwa rasmi kwa mara ya kwanza wakati wa msimu wa 2002/03.
5. Nacho Monreal
Ingawa mbali na Arsenal kuongeza uzuri zaidi enzi za Ligi Kuu England, wachache wamefanya kazi ngumu zaidi wakiwa wamevalia jezi nyekundu kuliko Nacho Monreal. Alipowasili kwa pauni milioni 8.5 kutoka Malaga mwaka 2013, aliendelea kukaa miaka sita na nusu akiwa na Washikabunduki hao, na alicheza zaidi ya mechi 250 na kushinda mataji matatu ya FA.
Beki huyo wa kushoto alikuwa mtumishi asiyechoka wakati wa kipindi kigumu kwa klabu hiyo, akivaa moyo wake kwenye mkono wake na kucheza zaidi ya mechi 35 katika kila msimu wake kamili. Aliondoka Emirates kama kipenzi kikuu cha mashabiki.
4. Emmanuel Adebayor
Emmanuel Adebayor na Arsenal hawakumalizana kwa maelewano mazuri. Baada ya kuondoka Kaskazini mwa London kuelekea Manchester City mwaka 2009.
Kukimbia kwa urefu wa uwanja na kupiga magoti mbele ya mashabiki wa Arsenal hakukuwa na uwezekano wa kupendwa na mashabiki wake, lakini mchezaji huyo wa Kimataifa wa Togo bado alikuwa usajili wa kuvutia alipojiunga na Washikabunduki hao mwaka 2006.
Alifunga mabao manne ya Ligi Kuu England katika kipindi chake cha kwanza cha nusu msimu na akafanikiwa kuongeza idadi hiyo mara mbili katika kampeni iliyofuata. Lakini ilikuwa wakati wa msimu wa 2007/08 ambapo alivutia sana, akifunga mabao 24 kwenye ligi katika mechi 36.
3. Theo Walcott
Theo Walcott aliipa Arsenal miaka 12 ya utumishi wa kutegemewa na wa kujitolea, na kuingiza jina lake katika vitabu vya historia ya klabu hiyo baada ya kuhamia London Kaskazini kutoka Southampton mwaka 2006. Hakuchukua muda mrefu kuongeza kasi ikizingatiwa alisajiliwa akiwa na umri wa miaka 16 pekee.
Winga huyo mwenye kasi aliichezea Arsenal mechi 382, akiifungia klabu hiyo mara 106, huku kampeni yake nzuri zaidi ikiwa ni ile ya msimu wa 2012/13. Alitikisa nyavu mara 21 na kutoa pasi 11 za mabao katika mashindano yote, na kuongeza jumla ya mabao 23 kutoka msimu uliofuata.
Ingawa zawadi ya mataji haikupatikana sana wakati wa uchezaji wake akiwa na Arsenal, Walcott alitwaa Kombe la FA mara mbili tofauti, hata kufunga katika fainali ya msimu wa 2014/15 wakati wa ushindi wa 4-0 dhidi ya Aston Villa.
2. Pierre-Emerick Aubameyang
Pierre-Emerick Aubameyang ndiye mchezaji aliyevunja rekodi ya Arsenal msimu wa 2017/18, akijiunga na klabu hiyo kwa pauni milioni 56. Matarajio yalikuwa juu sana kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Borussia Dortmund, ambaye alikuwa maarufu kwa ukatili wake mbele ya lango na kasi ya ajabu.
Tabia hizo zilionekana haraka pale Emirates alipofunga mabao 14 na kusaidia katika mechi nyingi katika miezi sita yake ya kwanza. Mchezaji huyo wa Kimataifa wa Gabon, aliboresha idadi hiyo msimu uliofuata, na kutwaa Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England kwa kufunga mabao 22.
Mabao hayakukauka katika kampeni zilizofuata na bao lao la kwanza kwa wakati muafaka ni katika fainali ya Kombe la FA msimu wa 2019/20 dhidi ya Chelsea ambalo liliihakikishia Arsenal ushindi.
Mzozo kati yake na kocha Mikel Arteta ulisababisha maisha yake ya soka ya Arsenal kuisha mapema, lakini anabakia kuwa mmoja wa wababe wa siku hizi wa klabu hiyo.
1. Martin Odegaard
Arsenal ilimsajili Martin Odegaard kwa mkataba wa kudumu wakati wa dirisha la majira ya joto, lakini awali alikuwa amejiunga na klabu hiyo kwa mkopo wa miezi sita Januari 2021.
Akiwa ametajwa kuwa nyota katika umri mdogo sana, uwezo wa Odegaard haukutosha kumhakikishia kucheza katika kikosi cha kwanza kule Real Madrid licha ya kucheza kwa mkopo mara kadhaa. Uhamisho wa muda kwenda Emirates ulimfanya kuinua mchezo wake na wababe hao wa Hispania walikuwa na furaha kuidhinisha dili la pauni milioni 30.
Odegaard amekuwa mtu wa mabadiliko katika chumba cha injini kwa Arsenal, akiongoza mapinduzi ya klabu chini ya Arteta. Sasa akiwa nahodha, ustadi wake, ubunifu na mguu wa kushoto umewasukuma Washikabunduki hao kwenye kilele cha ukuu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, ana muda mwingi wa kupambana zaidi kuacha urithi wake Arsenal.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED