Matajiri wanapojipeleka anga za mbali safari za kujirusha

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:49 AM Sep 17 2024

Wanaanga na mabilionea walioko safarini anga za juu; kutoka kushoto ni Anna Menon, Scott Poteet, Jared Isaacman na Sarah Gilli.
PICHA: REUTERS
Wanaanga na mabilionea walioko safarini anga za juu; kutoka kushoto ni Anna Menon, Scott Poteet, Jared Isaacman na Sarah Gilli.

INATAJWA kuwa ni safari hatari zaidi inayofanywa na mabilionea kutalii anga za mbali. Ikifanikishwa na chombo cha anga za juu cha kibinafsi Polaris Dawn, kilichoondoka duniani wiki iliyopita.

Kinaondokea Florida Marekani kikisaidiwa na roketi ya SpaceX Falcon 9, kikiwabeba bilionea Jared Isaacman, mwanzilishi mwenza wa kampuni ya malipo, Shift4, kwa mujibu wa BBC.

Pia yumo Scott "Kidd" Poteet, rubani mstaafu wa Jeshi la Anga la Marekani, na wahandisi wawili wa SpaceX, Anna Menon na Sarah Gillis.

Chombo hicho cha anga za juu, kiitwacho Resilience, kitaingia katika mzunguko wa kilomita 1,400 juu ya dunia.

Ikumbukwe hakuna binadamu aliyesafiri hadi sasa katika eneo hilo tangu mpango wa Apollo wa NASA ulipomalizika miaka ya 1970.

Wanaanga hao watapita katika eneo la anga za juu linalojulikana kama Van Allen Belt, lenye viwango vya juu vya mionzi, lakini watalindwa na chombo hicho chenye vifaa vyao vya kisasa vya anga za juu.

Kupita kwenye ukanda huo mara chache kutakuwa ni sawa na miezi na kupigwa na mionzi kwa miezi mitatu uzoefu walionao wanaanga kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga, ambacho kiko ndani ya mipaka inayokubalika.

Lengo la safari hiyo ni kujifunza madhara ya muda mfupi lakini salama ya mionzi kwa mwili wa binadamu.

Katika siku ya pili ya safari yao ya anga za juu wanaelezwa kuwa watafanya majaribio hadi 40, ikiwa ni pamoja na mawasiliano kati ya chombo cha anga za mbali cha Dragon na nyota ya setilaiti Space X.

KUVUNJA REKODI

Ikiwa mambo yote yatakwenda kama ilivyopangwa, siku ya tatu ya safari yao, Isaacman na Sarah Gillis wanatarajiwa kujaribu safari ya kwanza ya kibinafsi inayofadhiliwa, ambayo itadumu saa mbili angani.

Hii itafanyika wakati watakapokuwa kilomita 700 (maili 430) kwenye mzunguko, watajaribu mavazi mapya ya anga au suti za (EVA), ambazo, kama jina linavyoeleza, zimeboreshwa kulingana na shughuli za ndani za Space X (IVA) ili kufanya kazi nje ya chombo cha anga, wanaanga hao watakapohitaji kufanya shughuli hizo.

Mavazi yao yamebadilishwa kwa ajili ya kuhimili hali angani. Matangi ya ziada ya nitrojeni na oksijeni yamewekwa ndani ya chombo hicho na wanaanga wanne wanavaa mavazi mapya ya EVA, ingawa ni wawili watakaotoka nje ya chombo hicho kwa ajili ya kufanya uchunguzi.

Kwa hivyo ujumbe huo wa wanaanga utavunja rekodi ya idadi kubwa ya watu kuwahi kufika katika eneo lenye uwazi (vaccum) la anga za juu kwa wakati mmoja.

Wanaanga hao watafanya vipimo juu ya athari za ugonjwa wa decompression (matatizo yanayoweza kutokea kutokana na mgandamizo wa hewa), pamoja na hali ya wanaanga kushindwa kuona vizuri.

Jambo ambalo wakati mwingine huwapata wanapokuwa anga za juu, hali inayojulikana kama ‘neuro-ocular syndrome’.

VAZI JIPYA

Vazi la EVA linajumuisha kofia ambayo hutoa habari za sauti wakati liponavaliwa ni rahisi kuvaliwa wakati wa kuondoka na kutua duniani na kuondoa hitaji la vazi jingine.

Katika mahojiano yaliyofanyika wakati wa mafunzo kwa ajili ya safari ya anga za juu, Gillis anaelezea kuwa vazi hilo ni sehemu muhimu ya mipango ya Space X ya kupeleka watu kwenye sayari nyingine.

"Hadi sasa, ni safari za kitaifa tu ambazo zimefikisha watu anga za juu. Space X ina matarajio ya kufika katika sayari ya Mars na kufanya maisha kuwa tofauti.

Ili kufanikisha hilo, tunapaswa kuanzia mahali fulani. Na hatua ya kwanza ni kujaribu mwingiliano wa kwanza na nafasi ya EVA ili tuweze kuboresha zaidi nafasi na miundo ya suti ya baadaye."

 HATARI KUBWA

 "Kuna hisia kuwa kuna hatari nyingi zinazohusika," Dk. Adam Baker, mtaalamu wa roketi katika Chuo Kikuu cha Cranfield cha Uingereza, anaiiambia BBC.

"Wamejiwekea malengo mengi ya kutamani na matamanio mengi huku chombo chenyewe kikiwa ni kidogo . Kwa upande mwingine, wametumia saa elfu kadhaa kuinigia kwenye eneo linalolengwa. Kwa hivyo wanafanya kila wawezalo kupunguza hatari," mtaalamu huyo anasema.

Ikiwa safari hiyo itafanikiwa, baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa itachochea kufanyika kwa safari nyingine binafsi zenye gharama ya chini ambapo watu wengi wataweza kusafirishwa zaidi kuliko mashirika ya anga za juu ya serikali ambayo yamewahi kufanya hivyo.

Lakini Beker ana mawazo tofauti: "Mpaka sasa sekta binafsi imetumia fedha nyingi, imefanya matangazo mengi, lakini idadi ya watu ambao wamesafiri kwenda anga za juu na kurudi imekuwa chini ya 100."

"Safari ya anga za juu ni ngumu, ghali na hatari, kwa hivyo kutarajia kuona idadi kubwa ya raia matajiri wanaoruka angani wakati wowote hivi karibuni, au kuwa miongoni mwao, haiwezekani." Anaiambia BBC.

ANGA NA MATAJIRI

Kwa wengine, wazo la mabilionea kujilipia kwenda anga za juu ni la kusikitisha, na linaibua maswali mengi.

Simeon Barber, mwanasayansi wa anga za juu katika Chuo Kikuu Huria nchini Uingereza ambaye anatengeneza vyombo vya kisayansi kwa ajili ya anga za juu katika miradi inayofadhiliwa na serikali pekee, anasema sio jambo la ubatili.

"Isaacman ni mwanaanga mwenye uzoefu zaidi ni yeye pekee amekuwa angani hapo awali, kwenye safari nyingine inayofadhiliwa na SpaceX, ambapo pia aliwahi kuwa kamanda. Katika muktadha wa ujumbe huo,ni chaguo la asili," anakaririwa na BBC.

Anasema wengi katika sekta ya anga za juu wanaamini kuwa ushiriki wa watu matajiri ni jambo jema.

"Kama wanataka kujitosa kwenye mtandao, na siku moja kwenda mwezini au hata Mars, itatengeneza fursa za kisayansi. Na sababu tofauti zaidi za kuchunguza anga za juu, mpango huo utakuwa na nguvu na manufaa zaidi."