Bingwa afya akili, awaonesha vijana njia sahihi kukwepa madhara ngono

By Joyce Lameck , Nipashe
Published at 10:22 AM Sep 12 2024
Vijana katika mjumuiko wao. Ni mahali sahihi pa kupatiwa elimu ya afya yao na ngono.
PICHA: MTANDAO
Vijana katika mjumuiko wao. Ni mahali sahihi pa kupatiwa elimu ya afya yao na ngono.

KATIKA jamii nyingi, bado kuna imani ya kumpa elimu kijana kuhusu afya ya uzazi, kunachochea vishawishi vya kuanza ngono katika umri mdogo na kuwaletea madhara katika ukuaji wao.

Lakini, mzazi anatakiwa kukumbuka, pasipo elimu kwa kijana wake anaweza kupata elimu ya watu tofauti na kuangukia matokeo hasi kwa siku za baadaye.

Mbali na jamii inayomzunguka, kuna utandawazi ulioteka akili za vijana wengi sasa na huenda anaweza kujifunza vitu kupitia mitandao ya kijamii katika kupata darasa lolote analohitaji kujifunza.

Stahiki ya vijana ni kupatiwa elimu sahihi ya afya ya uzazi kupitia mtandao,  kuna sababu teknolojia inayokua kwa kasi duniani na vijana wengi wanaitumia kutoa au kupokea taarifa mbalimbali.

Baadhi ya mitandao imekuwa ikitoa elimu isiyo sahihi kwa vijana na wanaamua kwa njia isiyo sahihi, kuhusu mambo ya uzazi salama na hata kuleta madhara kwa kundi kubwa la vijana.                      

Ili wapate taarifa sahihi za afya ya uzazi, wanapaswa kufuatilia idhaa za radio au televisheni zinazotoa zaidi elimu na sio habari zile za udaku, kwa sababu mara nyingi vinaandaliwa vipindi maalumu vya kuelimisha.

BINGWA AELEZ A 

Mratibu wa Kitaifa wa Masuala ya Afya ya Uzazi wa Vijana na Jinsia, Dk. Gerald Kihwele, alisema kuwa vijana wanapaswa kupata taarifa sahihi kutoka kwenye idhaa sahihi kwani hiyo ni changamoto kubwa inayowakumba vijana.

Msomi huyo wa afya ya akili, mwenye umri ulioko ‘mitaa ya ujana’ na uzoefu wa kutumika katika Hospitali ya Afya ya Akili Mirembe, jijini Dodoma, ana ushauri  kwa watoa huduma za afya, watumie idhaa zinazopendwa na vijana za  redioni,  kuwafikisha elimu hiyo kirahisi.

Anaitaja kuwa staili bora, maana somo hilo hilo redioni au kwenye televisheni kuhusu afya ya uzazi, mara nyingi zinakuwa na watu maarufu, wenye weledi na wepesi kufanikisha uelewa wao. 

Dk. Kihwele anasema, wazazi wanapaswa kutafuta namna ya kuzungumza na vijana wao, jinsi ya kutumia mitandao hata kuweza kupata elimu kuhusu afya ya uzazi na si kuwekea mazingira ya kuwafanya vijana kuona suala hilo ni kosa.  

Kipindi cha umri wa ama balehe au ‘binti kuvuka awamu ya kwanza’ ni mabadiliko ya kimwili, kitabia na kihisia, hata wanapofanya uamuzi wanakuwa na taarifa za kutosha kuhusu afya yao ya kingono, sambamba na mabadiliko hayo ya afya ya uzazi.

Eneo lingine analolitaja mtaalamu huyo, ni haja ya kijana anapoangukia stahiki ya kufikiwa na maarifa, vilevile ujuzi unaohusiana na huduma za afya, anakuwa katika nafasi bora na wenye taarifa sahihi za afya, pia uzazi salama unaogusa maisha ya ngono.

Ni taarifa zinazowasaidia vijana kuchelewa kuanza vitendo vya ngono, wakihitaji pia ‘kingamimba’ wakati wanapoamua kufanya ngono. Vyote vinajielekeza katika namna ya kuwa na taarifa zinazomfaa kiumri, kuhusu ngono salama na afya bora ya uzazi na ukuaji wake.

Ngome ya taarifa tajwa inagusa uhusiano, maadili, mtazamo, stadi, utamaduni, jamii na haki za binadamu katika ukuaji, zikigusa mwenendo wa kingono na afya ya uzazi, vijana kupata uelewa unaowahusu.

Kisaikolojia na kijamii, watoa huduma wanahitaji kuhakikisha vijana wanapata maarifa na huduma wanazozihitaji, ili kujilinda na wengine dhidi ya madhara yasiyokusudiwa kingono, ikiwamo maambukizo ya magonjwa ya zinaa na mimba zisizotarajiwa.

Wataalamu wanataja nafasi nyingine wanayopsawa kupewa vijana, ni ushauri kuhusu maisha ya balehe, viungo vya uzazi, ngono, mzunguko na mwenendo wa wa maisha ya kingono na mwitiko wake, vyote vitawasaidia kuwa makini kufanya uamuzi sahihi.

UZUIAJI MIMBA

Katika jukumu la kuzuia mimba, suala la kutoa kingamimba za dharura, pia kuelewa, kutambua na kupunguza uwezekano wa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) ni muhimu.

Ukuaji teknolojia duniani, inawafanya watu wengi sasa wanatumia mitandao katika utoaji elimu tofauti, zinazosaidia jamii kupata uwelewa wa kutosha  unaohusu masuala mbalimbali.

Hata hivyo watoa huduma za afya ni vema wakatumia mitandao katika kutoa elimu na mafunzo kuhusiana na afya ya uzazi, kwani kwa sasa si rahisi kijana kwenda hospitali kwa ajili ya kupata elimu juu ya uzazi. 

vijana wakiwa katika hatua, bado hawajaitwa baba au mama, inawafanya wengi kushindwa kupata elimu sahihi ya uzazi na kuwawezesa kufikia uzazi salama.

Elimu ya Afya ya Uzazi kwa vijana inawapatia maarifa ya kujitambua, kufahamu mabadiliko yanayoweza kuwatokea pindi wanapoendelea kukua na namna ya kufanya maamuzi sahihi kwa kuwa hali ya kukosa elimu sahihi ya uzazi imekuwa ikileta madhara.

Kuna vijana sasa wanapata mimba, wakati hawana elimu sahihi ya uzazi, ilhali wana na ‘simu janja’. Hivyo, kuwapo makundi sahihi ya vijana mitandaoni, yanasaidia vijana wengi kupata taarifa sahihi juu ya afya ya uzazi na  kutokomeza dhana za kizamani kuhusu uzazi.

Vile vile kuwapo na majukwaa ya kidijitali katika mitandao, yanayozungumzia afya ya uzazi salama kwa vijana na kuwapa fursa ya kuuliza maswali na ufafanuzi sahihi, nayo yana umuhimu wake.

Mustakabali mpana wa elimu ya uzazi kwa vijana, inmavuta majibu na haki kwao kuyajua, hivyo washirikio kuyadhibiti magonjwa mengi ya zinaa nchini, kama vile kaswende na Ukimwi.