WAUGUZI na wakunga 90 wa mkoa wa Shinyanga, wamepewa mafunzo ya vitendo kuhusu utoaji wa huduma za dharura, kwa akinamama na watoto wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.
Wauguzi hao ni kutoka katika Hamashauri ya Manispaa ya Kahama, Kishapu, Wilaya ya Shinyanga pamoja na halmashauri ya Ushetu na mafunzo hayo ni utekelezaji wa mradi wa Dhamini uzazi salama unaofadhiriwa wa watu wa Canada.
Mwakilishi wa UNFPA nchini, Dk. Sande Rwebangile, ameyabainisha haya leo, kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika Manispaa ya Kahama, lengo likiwa ni kukabiliana na vifo vya wajawazito na watoto.
Amesema awamu ya kwanza ya wauguzi na wakunga 30 wameshapewa mafunzo hayo na malengo la utoaji wa mafunzo hayo ni sehemu ya kuboresha ujuzi kwa wauuguzi na wakunga katika kutoa huduma, ili kuwafanya wajawazito kujitokeza na kujifungulia kwenye vituo vya afya au hospitali.
Dk. Sande amesema, mradi huo unatarajia kuwafikia wajawazito milioni moja, watoto wadogo 800,000, wanufaika ambao sio wa moja kwa moja milioni nne na wanajamii zaidi ya 500,000 katika mkoa wa Dar es Salaam na Shinyanga.
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga, Ziada Sellah, amesema mpaka sasa wameshawafikia wauguzi na wakunga 5,863 kutoka mikoa 13 ya Tanzania bara na kuwapatia elimu ya utoaji huduma kwa wajawazito na watoto na imesaidia kupunguza vifo vitokavyo na uzazi.
Amesema, kukosekana kwa ujuzi ndio sababu kubwa inayosababisha kutokea kwa vifo hivyo na hii ndio sababu kubwa ya mashirika na serikali ya Canada kutoa mafunzo hayo, ili kufikia azma ya serikali katika mapambano ya vifo vya wajazito na watoto.
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Saitore Laizer, amesema asilimia 30 ya wajawazito, bado wanajifungulia majumbani na kusaidiwa na watoa huduma ngazi ya jamii na kuwataka kuongeza juhudi ya kutoa elimu.
Amesema, mpaka mama yake mzazi anazeeka na kukosa nguvu alikuwa mtoa huduma ngazi ya jamii kwa kuwazalisha wajawazito majumbani na hata alipokuwa anasoma MUHAS, alikuwa anamuunga mkono mama yake kwa kumnunulia ,gloves’ ili kujikinga na maambukizi.
Dk. Laizer amesema, serikari kupitia Dk. Samia Suluhu Hassan, ameboresha huduma za afya kila kona, vifaatiba na dawa, hivyo hakuna sababu ya wajawazito kuendelea kujifungulia majumbani, hivyo wanapoanza kliniki wakumbushe umuhimu wa kujifungulia kwenye vituo vya afya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED