TANROADS kutekeleza miradi 11 Dar, kupunguza foleni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:50 PM Mar 14 2024
Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam Mha. John Mkumbo.
PICHA: MPIGA PICHA WETU
Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam Mha. John Mkumbo.

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam Mha. John Mkumbo amesema katika kipindi cha miaka mitatu serikali imetekeleza zaidi ya miradi 11 katika mkoa huo kati ya hiyo miradi nane ni mikubwa ya kimkakati na mitatu ni midogo ambayo itasaidia kutatua changamoto za barabara kutopitika vizuri na kupunguza msongamano wa magari.

Akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika Sekta ujenzi wa miundiombinu ya barabara na Madaraja; Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar- es Salaam Mha. Mkumbo amesema kati ya miradi hiyo, miradi mitano imekamilika na sita inaendelea kutekelezwa.

Amesema miongoni mwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa ni pamoja na mabasi ya mwendo wa haraka awamu ya pili (BRT 2)  katika barabara ya Da- es Salaam – Kongowe eneo la Mbagala Rangi tatu, Chang’ombe (Keko- Mgulani JKT), Kawawa (Veta Chang’ombe JCT- Magomeni Mapipa) na Sokoine ambapo mradi umefikia 98%.

Amesema ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo haraka Awamu ya tatu (BRT 3) km 23 katika barabara ya Tanganyika Motors – DIA TI, Uhuru (Buguruni – Msimbazi ) Bibi titi na Shauri moyo ( Karume – Bohari), unaendelea  pamoja na ujenzi wa miundombinu ya Mabasi yaendayo haraka awamu ya nne (BRT 4) unaoanzia maktaba ya Taifa – Mwenge – Sam Nujoma km 13.5 ambao unapita pia katika barabara ya Mwenge – hadi (DAWASA) Tegeta km 15.63.

Pia kuna utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa barabara ya Morogoro kutoka njia mbili kwenda njia nane km 19 na maegesho ya magari Kiluvya yenye urefu wa mita za mraba 36,000 awamu ya kwanza ikihusisha ujenzi wa maegesho yenye ukubwa wa mita za mraba 18,000 yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua wastani wa malori zaidi ya 200 kwa siku, lengo ni kuondoa maegesho yasiyorasmi pembezoni mwa barabara ya mandela na hivyo kupunguza foleni zinazoweza kuepukika.

Ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara ikiwemo matengenezo ya muda maalum, matengenezo ya kawaida, matengenezo ya maeneo korofi na matengenezo ya madaraja ambapo kazi hizo zimekuwa zikitekelezwa na Wakandarasi wazawa ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/ 2024 jumla ya miradi 33 imetekelezwa na Wakandarasi wazawa.