UCHAGUZI wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), ambao umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu siku za hivi karibuni, umefanyika mwishoni mwa wiki na Mahamoud Ali Youssouf Ali Youssouf, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Djibouti kushinda.
Ulikuwa uchaguzi wenye ushindani, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Djibouti, Youssouf meibuka mshindi dhidi ya Raila Odinga, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya na Richard Randriamandrato, Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Madagascar.
Youssouf alishinda kwa kupata kura 33 katika raundi ya saba, ambayo alisalia kama mgombea pekee, baada ya Raila kujiondoa katika raundi ya sita, kufuatia kupitwa kura na Youssouf katika raundi ya tatu, nne, tano na raundi hiyo ya sita.
Randriamandrato kutoka Madagascar, waziri mambo ya nje wa zamani alijiondoa katika raundi ya tatu.
Youssouf, sasa anakwenda kumrithi Moussa Faki Mahamat, kama mwenyekiti mpya wa Tume hiyo ya Umoja wa Mataifa kutoka Chad, mwanadiplomasia aliyechaguliwa kushika wadhifa huo tangu Machi 14, 2017.
MAHAMOUD ALI YOUSSOUF NI NANI?
Mahamoud Ali Youssouf (58), ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi ndogo ya Djibouti, yenye umuhimu wake kimkakati katika Pembe ya Afrika.
Ni mwanadiplomasia na msomi mwenye taaluma ya uongozi wa biashara akisomea chuo kikuu cha Liverpool nchini Uingereza.
Mbali na kushika ubalozi wa Djibouti nchini Misri kati ya mwaka 1997 na 2001, amekuwa waziri wa mambo ya nje wa Djibouti tangu 2005, akihudumu chini ya marais watatu.
Ndiye Waziri anayetajwa kushika wadhifa wa mambo ya nje kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.
Kushika kwake wadhifa huo muhimu katika siasa kwa miongo miwili inakuonyesha ni mtu wa aina gani.
Ni mtu mwenye kuungwa mkono anayeonyesha dhamira ya kufanya kitu kwa taifa lake na bara la Afrika.
"Lengo langu kuu nikichaguliwa ni kukomesha kuenea" kwa virusi katika bara hilo, aliiambia AFP katika mahojiano mwezi uliopita.
Alisema kuwa kamati hiyo inahitaji marekebisho, na kuongeza kuwa mageuzi haya yaanze kwa uongozi na viongozi wakuu.
Mbali na kudumisha amani na usalama barani humo, alisema matarajio yake ni kukuza maendeleo ya kiuchumi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Anajivunia kuwa na uwezo wa kuzungumza lugha mbalimbali na anaamini kwamba uwezo huu wa kuwasiliana unamwezesha kuwa daraja linalounganisha kaskazini na kusini, mashariki na magharibi.
SIKU 100 OFISINI
Wiki chache akiwa jijini Dar es Salaam, akizungumza na waandishi wa habari, Youssouf, akiwania nafasi ya uenyekiti Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), alisema iwapo atachaguliwa, vipaumbele vyako vitajikita maeneo sita, ikiwamo uwekezaji kwenye teknolojia kurahisisha upatikanaji mtandao na bei nafuu hadi vijijini barani Afrika.
Youssouf, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na na Ushirikiano wa Kimataifa Djibouti, amesena katika siku 100 ofisini atazingatia pia vipaumbele vingine ambayo ni kilimo, uchumi, afya, miundombinu, ili kuliondoa bara hilo kwenye utegemezi wa ki loluchumi.
Alisema anawania nafasi hiyo pamoja na wagombea wengine, akieleza kwamba anafaa kutokana na uzoefu wake kidiplomasia.
"Nitazibadili changamoto kuwa fursa. Nina uzoefu wa kutosha kutokana na uzoefu nilionao. Niishinda nitawezesha upatikanaji wa intaneti na wa bei rahisi hadi vijijini, ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia duniani.
"Kunahitajika kuzuia migogoro, huko Libya, DRC (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), Sudan, Sahel, pamoja na mimi binafsi nitazingatia hilo, nitahakikisha eneo la kulinda amani na kuitunza linafanya kazi," alisema.
Alisema bara la Afrika linahitaji jeshi imara, ili inapotokea dharura lifanye kazi na kwamba usalama wa bara hilo, kutawezesha kufikia lengo la Afrika tuitakayo ifikapo 2063.
Kwa upande wa kilimo alisema kunahitajika uwekezaji na mnyororo wa thamani wa mazao, ili malighqfi zinazopatokana zilinufaishe bara.
"Kuna vikwazo vya kiuchumi, miundombinu, mipakani, usafiri wa anga pia. Biashara zetu zinakuwa za msongamano sana hatuna usafiri wa anga wa uhakika na wa kutosha.
“Kunahitajika uchumi wa kikanda wa pamoja. Tuna nguvu ya kutoka barani ambako asilimia takribani 60 ni vijana. Kwenye mabadiliko ya tabianchi, tunahitaji sauti ya pamoja katika uwakilishi wa ili kufikisha ujumbe wetu duniani,” alisema Youssouf.
Kadhalika, alisema kuhusu uwakilishi wa wanawake kwenye nafasi za maamuzi ni muhimu hivyo atakaposhinda atazingatia jinsia huku akisisitiza Afrika ijayo ni ambayo iko huru kwenye eneo la afya hasa kuwa na uzalishaji wa dawa na chanjo.
Umoja wa Afrika (AU), ulitoa majina ya wagombea wanne wanaowania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Wagombea walioidhinishwa ni kutoka mataifa ya Afrika ikiwa ni pamoja na Kenya, Djibouti, Mauritania na Madagascar. Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC0), zimepewa nafasi ya kutoa mrithi wa mwenyekiti wa sasa Mousa Faki, raia wa Chad, ambaye amekuwa akishikilia wadhifa huo tangu mwaka 2017.
NYONGEZA BBC
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED