Serikali yaweka wazi uwekezaji bandari Bagamoyo

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 08:42 AM Feb 16 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo
PICHA: MTANDAO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo

SERIKALI imesema kwa sasa haijaingia makubaliano na mwekezaji yeyote kwa ajili ya kujenga na kuendesha Bandari ya Bagamoyo.

Pia serikali imesema taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa imeingia makubaliano na kampuni kutoka Saudi Arabia hazina ukweli.

 Juzi, katika mitandao ya kijamii, ilidaiwa kuna kampuni moja  kutoka Saudi Arabia imepata mkataba wa uwekezaji wa kujenga na kuendesha bandari hiyo.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo alitoa ufafanuzi wa jambo hilo juzi bungeni alipopewa nafasi na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, kueleza umma ukweli kutokana na taarifa zinazopita mitandaoni kusababisha sintofahamu.

 Akitoa ufafanua kuhusu uendelezaji wa eneo maalum la kiuchumi la Bagamoyo (BSEZ), Prof. Mkumbo alisema serikali iko katika hatua mbalimbali za kutekeleza programu ya ujenzi wa eneo hilo ikiwa ni moja ya miradi 17 ya kielelezo iliyopo katika Mpango wa Tatu  wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26. 

 “Pamoja na mambo mengine, programu ya ujenzi wa Eneo Maalum la Kiuchumi  la Bagamoyo (BSEZ) itahusisha ujenzi wa Bandari, Kongani za Viwanda, Kongani za TEHAMA, Ukanda huru wa Biashara, na Kituo cha reli,”alisema.

 Alisema utekelezaji wa programu hiyo utafanywa na sekta binafsi kwa kushirikiana na  serikali kupitia mpango wa ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (PPP).

 “Wakati wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wameonesha nia ya  kuwekeza katika ujenzi wa miradi mbalimbali iliyopo katika programu ya BSEZ,  na wapo katika hatua mbalimbali za mazungumzo na taasisi mbalimbali husika za serikali.

 “Serikali haijaingia makubaliano yoyote wala mkataba na mwekezaji yeyote kwa sasa kuhusu mradi wa Bagamoyo ikiwamo Bandari hivyo, taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kwamba kampuni moja  kutoka Saudi Arabia imepata mkataba wa uwekezaji wa kujenga na kuendesha  Bandari ya Bagamoyo sio za kweli,”alisema.

 Alisema kutokana na umuhimu na ukubwa wa programu ya BSEZ, umma utajulishwa kikamilifu katika kila hatua ya utekelezaji wake.