Serikali yajidhatiti kuboresha huduma za kijamii

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 10:42 AM Feb 16 2025
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa
PICHA:MPIGAPICHA WETU
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za elimu, maji na afya ili kuboresha maisha ya wananchi.

Akizungumza leo wilayani Maswa, mkoani Simiyu wakati wa mkutano mkuu wa jimbo la Maswa Mashariki, Majaliwa ameeleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora katika maeneo yao.

Katika sekta ya elimu, Waziri Majaliwa amesema kuwa serikali imeendelea kujenga shule za msingi na sekondari katika maeneo yaliyokuwa na upungufu mkubwa wa miundombinu hiyo.

"Tumejenga shule za sekondari katika maeneo ambayo hapakuwa na shule, tumeongeza vyumba vya madarasa pale palipohitajika, na tumepandisha hadhi baadhi ya shule za sekondari za chini kuwa sekondari za juu. Kazi hii inaendelea, na mbunge wenu bado anasimamia kikamilifu kuhakikisha elimu bora inawafikia wananchi," amesema Majaliwa.

Ameongeza kwa kubainisha kuwa serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kila kijiji na kitongoji kinapata huduma ya maji safi na salama, kwa kuchimba visima na kuweka mitandao ya mabomba.

"Maji huwa hayatoshi mpaka yanapoingia ndani ya nyumba. Mkakati wa serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata maji bila kutembea umbali mrefu. Tumekuwa tukitumia teknolojia ya kuvuta maji kutoka maziwa makubwa kama Victoria, Tanganyika na Nyasa ili kuhakikisha maji yanawafikia wananchi," amesema Majaliwa.

Ameeleza kuwa mradi mkubwa wa maji kutoka Busega hadi Maswa ni sehemu ya jitihada hizo, na kwamba serikali imepanga kufikisha maji kwenye wilaya zote, makao makuu ya mkoa wa Simiyu na vijiji.

Katika sekta ya afya, Majaliwa amesema kuwa lengo la serikali ni kupunguza gharama za wananchi katika kupata huduma za afya kwa kujenga na kuimarisha miundombinu ya afya.

"Tunaendelea kujenga zahanati, vituo vya afya na kuimarisha hospitali za wilaya. Hospitali yenu hapa Maswa imeboreshwa, tumeongeza jengo la dharura, na huduma zimeimarishwa ili wananchi wasiwe na mashaka yoyote wanapohitaji matibabu," amesema Majaliwa.

Akimzungumzia Mbunge wa Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo, amesema ni mtaalamu wa afya ambaye amekuwa akifanya kazi kubwa kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa katika wilaya hiyo.

"Mbunge wenu ni mtaalamu wa afya na amekuwa akihakikisha huduma hizi zinaimarishwa. Endelea kuwatumikia wananchi, yale mapendekezo uliyoyaleta kuhusu kuongeza vituo vya afya na zahanati tutayafanyia kazi," amesisitiza Majaliwa.