Sendiga awabana TARURA, TANROADS

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 04:44 PM Feb 17 2025
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga akizungumza kwenye kikao cha Bodi ya Barabara
Picha: Jalliwason Jasson
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga akizungumza kwenye kikao cha Bodi ya Barabara

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amesema Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini(TARURA), kama hawajajipanga wasiingie makubaliano na wakandarasi.

Sendiga ametoa kauli hiyo leo, Februari 17, 2025, katika kikao cha Bodi ya Barabara, kwa mwaka wa fedha 2025/26 akisema iwapo serikali haina fedha ni bora kutosisaini mikataba ya ujenzi wa barabara na wakandarasi, ili kuepuka lawama kutoka kwa wananchi.

"Wananchi wa sasa hivi ni waelewa sana lazima wahoji wakiona kazi haiendelei wakati tunakuwa tumeishasaini mikataba, huwezi kuwaambia wananchi kuwa hatuna fedha," amesema Sendiga

Akichangia kwenye kikao hicho, Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Masaay, amesema hali ilikuwa ngumu kutokana na miradi mikubwa na makusanyo kuwa madogo.

Sendiga awabana TARURA, TANROADS
Masaay, amesema deni la taifa nalo kuongezeka ni miongoni mwa sababu zinazosababisha hali kuwa ngumu kwa serikali.

Vilevile amesema ameanza kuogopa kuongea juu ya ujenzi wa barabara, kutokana na kila akiongea mawaziri wa ujenzi wanaondolewa kwenye hiyo nafasi.

Awali akitoa taarifa ya TANROADS Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara, Dutu Masele, amesema miongoni mwa  changamoto zinazowakabili ni ufinyu wa bajeti na wakandarasi kutokulipwa kwa wakati na kusababisha kukwama kwa miradi.

Wakati huohuo Mkuu wa Mkoa, ameunda kamati maalum ya kujadili namna ya kuwa na barabara ya dharura wakati likijengwa daraja la Msasani, lililopo barabara kuu ya Babati/Arusha.

Sendiga awabana TARURA, TANROADS
Sendiga amesema akatika kamati hiyo awepo Meneja wa TANROADS Mkoa, Meneja wa TARURA Wilaya ya Babati, Diwani wa Kata ya Maisaka, Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Mkoa wa Manyara, Anna Ulomi ambaye ni mfanyabiashara wa Babati na Mkuu wa Usalama wa Wilaya ya Babati na Mkuu wa Usalama Barabarani (RTO) mkoani hapa.

Mkuu huyo amesema ikiwezekana aongezwe Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul, na kamati hiyo inatakiwa kufanya kazi na kuwasilisha taarifa Februari 19, mwaka huu.

Lengo la kamati hiyo ni kushirikisha viongozi na wananchi katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.