PM aonya watoa misaada wachonganishi

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 08:47 AM Apr 18 2024
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na waathirika wa mafuriko.
PICHA: MAKTABA
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na waathirika wa mafuriko.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameonya tabia ya baadhi ya wadau wanaotoa misaada kwa waathirika wa mafuriko Rufiji mkoani Pwani na kuwataka kuacha mara moja kupotosha na kuwachonganisha wananchi na serikali.

Akizungumza baada ya kutembelea waathirika hao katika kambi ya Chumbi  wilayani Rufiji, amesema suala la mafuriko ni kubwa na halipaswi kufanyiwa mzaha, hivyo tabia ya kuwachanganya na kuwapotosha wananchi juu ya chanzo chake si sahihi na serikali haiwezi kufumbia macho.

Baadhi ya wadau, amesema wamekuwa wakifika katika maeneo hayo na kutoa matamshi yanayoudhi kwamba chanzo cha mafuriko hayo ni ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, jambo ambalo si sahihi kutokana na ukweli kwamba eneo hilo limekuwa likikumbwa na mafuriko kwa miaka yote.

"Tunatambua michango na misaada inayotolewa na wadau mbalimbali lakini tunaomba msije kuwapotosha na kuwachanganya wananchi juu ya chanzo cha mafuriko. Nimetoka  Morogoro mafuriko ni mengi. Je,  pale pana bwawa? Mafuriko  hapa yapo miaka yote na hali imekuwa hivi kutokana na wananchi kujenga mabondeni," amesema.

Pia amesema serikali kupitia kamati ya maafa kitaifa, iko kazini kuhakikisha waathirika wote wa mafuriko nchini wanapata huduma mbalimbali zikiwamo chakula, maji safi na afya pamoja na kuwatafutia maeneo salama kwa ajili ya makazi.

Waziri Mkuu amesema baadhi ya watu wasio waaminifu wamekuwa wakijichanganya na waathirika kwa lengo la kujipatia misaada mbalimba jambo ambalo si sahihi. Aliwaagiza watendaji wa vijiji na wenyeviti kuwatambua wananchi wao ili kuondoa mkanganyiko.

"Watendaji wa vijiji na kata mshirikiane na kamati hizi za maafa kuwatambua watu walioathirika ili tuache kuhudumia watu ambao hawajapata maafa na kuwawezesha wahusika kuhudumiwa na kunufaika na misaada hii," amesema.

Pia ameziagiza serikali za vijiji katika maeneo yote yaliopata maafa nchini kutafuta maeneo mazuri yenye miinuko ili kuwahamishia wananchi katika maeneo hayo na kwamba maeneo ya mambondeni yatunike kwa kilimo na si makazi.

"Niwasihi wananchi mwendelee kusikiliza serikali na maelekezo tunayotoa mvua bado zipo  na kila siku zinanyesha na Mamlaka ya Hali ya Hewa imesema mvua zipo mpaka mwezi Mei, hivyo walioko mabondeni waendelee kuchukua tahadhari ikiwamo kuondoka katika maeneo hayo," amesema.

Majaliwa pia ameziagiza kamati za maafa kuhakikisha misaada yote inayotolewa na serikali na wadau mbalimbali inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa sambamba na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) kuimarisha miundombinu ya barabara.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya waathirika hao, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema kwa sasa hali ni nzuri na kwamba wananchi wanaendelea kupata huduma mbalimbali ikiwemo za afya.

"Waathirika tulio nao hapa ni zaidi ya 2,880 na katika kambi hii, wako 411. Huduma  zinaendelea kutolewa kama kawaida na misaada bado inahitajika. Naomba  wadau waendelee kujitoleza," amesema Kunenge.