Nyuki wazua taharuki, wajeruhi wanafunzi 17

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 08:58 AM Apr 18 2024
Nyuki.
PICHA: MAKTABA
Nyuki.

KUNDI la nyuki limevamia Shule Shikizi ya Mjiha, Manyoni mkoani Singida na kujeruhi wanafunzi 17 ambao walipelekwa katika Zahanati ya Kijiji cha Heka kwa ajili ya matibabu.

Tukio hilo limetokea wakati wanafunzi hao wakiwa darasani wakiendelea na masomo ndipo kundi la nyuki lilipovamia shule hiyo na kuanza kuwashambulia wanafunzi na walimu ambao kila mmoja alianza kukimbilia vichakani kujihami.

Mmoja wa walimu wa shule hiyo, Hadija Selemani,  akizungunza wakati Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni, Jumanne Makhanda, alipotembelea kuwapa pole wanafunzi hao, alisema uvamizi wa nyuki hao ulizua  taharuki kubwa na kuingilia shughuli za masomo. 

"Nyuki walipovamia shule wanafunzi walianza kukimbia ovyo kwenda vichakani kunusuru maisha yao, lakini wakati huo wako ambao tayari walikuwa wamejeruhiwa kwa kung'atwa na nyuki hao," amesema.

Selemani amesema baada ya tukio hilo, wanakijiji walianza kupiga yowe na wengine kufika shuleni hapo kuokoa watoto na baada ya muda, kundi hilo la nyuki liliondoka katika mazingira ya shule.

Amesema wanafunzi 17 ambao walikuwa wamejeruhiwa walichukuliwa haraka na kupelekwa katika zahanati ya Heka kwa ajili ya matibabu.

Mwenyekiti Makhanda alifika katika zahanati ya Kijiji cha Heka kuwapa pole wanafunzi hao ambao walikuwa wakiendelea kutibiwa na kutoa pesa za kuwanunulia vinywaji na vitafunwa.

"Kwa niaba ya CCM nawapa pole sana kwa tukio hili na zahanati hii pamoja na kwamba ni ndogo lakini imeweza kuwahudumia wanafunzi hawa tumeambiwa na wahudumu dawa zipo watahudumiwa vizuri," amesema.

Makhanda amesema kama itatokea kuna mwanafunzi hali yake itakuwa mbaya zaidi, gari la CCM ambalo lililala katika Kijiji cha Heka litakuwa tayari kumchukua na  kumpeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni kwa matibabu zaidi.

Mwenyekiti huyo pia amesema wazazi wasilazimishe kuwachukua watoto wao kurudi nao nyumbani kama wanafunzi hao watakuwa hawajatibiwa na madaktari kujiridhisha kuwa wamepona.